Serikali kuongeza ndege 2 aina ya Airbus

20Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali kuongeza ndege 2 aina ya Airbus

SERIKALI imesaini mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine mbili mpya na aina ya Airbus zitakazokuwa na muundo wa A220-300 zilizoboreshwa.

Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege (ATCL), Ladislaus Matindi.

Makubaliano hayo yalifanyika katika ya Serikali na Mwakilishi wa Kampuni ya Airbus ya nchini Canada kwa lengo la kuongeza ndege hizo.

Tayari serikali imeshanunua ndege sita ambazo zinafanya kazi, mbili aina ya Dreamliner na Bombardier zinazotarajiwa kuingia nchini mwezi Oktoba au Novemba, mwaka huu.

Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege (ATCL), Ladislaus Matindi, akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, alisema makubaliano hayo yamewekewa uzito wa kisheria na kutoa haki kwa serikali kuanza kufuatilia ndege hizo.

Alisema ndege hizo zitakuwa na muonekano wa tofauti kwa kuwekewa runinga kwa ajili ya kuongeza mvuto wa kibiashara na kuwapa wateja burudani.

"Makubaliano haya yanatupa uzito wa kesheria wa kuanza kufuatilia na wao kuanza kutengeneza ndege hizi ambazo tumezifanyia maboresho kwa kuweka runinga tofauti na za awali lengo ni kuwapa burudani wateja wetu," Matindi alisema.

Alisema serikali inaendelea kufuatilia hali ya usalama katika nchi ya Afrika Kusini kabla ya kuanza kuruhusu safari za ndege zilizositishwa kutokana na kuwapo kwa machafuko.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali, Dk. Benjamin Ndimila, aliyesaini mkataba huo kwa niaba ya serikali, alisema serikali inajenga historia kupitia utendaji kazi wa Rais John Magufuli ambaye ni dira kuu ya kutekeleza hayo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Mauzo wa Kampuni ya Aibus ukanda wa Afrika na Asia, Hadi Akoum, alisema baada ya kuingia makubaliano hayo, wanatarajia kukamilisha ujenzi wa ndege hizo ndani ya mwaka mmoja hadi mmoja na nusu.

Alisema kuwapo kwa ndege hizo nchini kunaendelea kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya utalii na biashara.

Aliipongeza serikali kwa kukamilisha jengo la tatu la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kusema kuwa ni kivutio kinachochea uchumi wa taifa.

Sifa ya Airbus

Ndege hiyo, ambayo inaundwa na kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus, itakuwa ya muundo wa A220-300.

Airbus A220 zilikuwa zinafahamika kama Bombardier CS100s kabla ya Airbus kuununua mradi huo wa utengenezaji wa ndege za C Series.

Ina urefu wa mita 38.7, na kwa jumla inaweza kuketi abiria 141, urefu kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa ni mita 35.1.

Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa 5,920km safari moja, na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.

Ndiyo ndege kubwa miongoni mwa familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safari za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.