Tigo yaahidi makubwa IPP

20Sep 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tigo yaahidi makubwa IPP

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Tigo, imeahidi kuongeza ushirikiano wa kibiashara na vyombo vya habari vya IPP na kukuza ukaribu uliopo sasa.

Ofisa Biashara Mkuu wa Tigo, Tarik Boudiaf.

Ofisa Biashara Mkuu wa Tigo, Tarik Boudiaf, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika vyombo vya habari vya IPP.

"Tuna imani katika ushirikiano na tunahitaji ushirikiano. IPP ni moja ya washirika wetu katika biashara. Tunaahidi kuendeleza ushirikiano, nasi tunahitaji ushirikiano wenu na tunaomba tuendeleze ushirikiano," alisema Boudiaf.

Akiwa katika ziara hiyo, Boudiaf aliahidi kampuni yake kutoa ushirikano wa baadhi ya huduma kama vile vifurushi vya kuperuzi vitakavyowasaidia waendesha vipindi na watangazaji kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

"Nimefurahi kutembelea vyombo vya habari vya IPP. Sikutarajia kuona IPP ni kubwa sana. Katika ziara yangu hii nimeongeza maarifa katika masuala ya habari," alisema Boudiaf.

Kwenye ziara hiyo, Boudiaf ambaye aliambatana na Ofisa Mawasiliano wa Tigo, Umi Mtiro, walitembelea The Guardian Ltd na kuona namna uzalishaji na uandaaji wa habari unavyofanyika.

Pia walitembelea vituo vya runinga na redio vya EATV, East Africa Radio, Radio One, Capital Televisheni ITV.

Habari Kubwa