Mjadala kura polisi kabla uchaguzi

20Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mjadala kura polisi kabla uchaguzi

SUALA la vikosi vya ulinzi na usalama kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi, limepokewa kwa mitazamo tofauti huku baadhi ya vyama vya siasa vikionyesha hofu.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga.

Wakati mjadala ukiibuka juu ya sakata hilo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imetoa ufafanuzi juu ya suala hilo ambalo limesababisha mjadala mzito miongoni mwa wadau.

Huku hali ikiwa hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka bayana kwamba hakuna ubaya wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo kikisema huenda ni njama za kuwakandamiza wapinzani.

CCM kupitia Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, imeunga mkono suala hilo na kusisitiza kuwa jambo hilo ni zuri kutokana na dhamana watakayokuwa nayo askari hao siku ya uchaguzi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari katika warsha ya viongozi wa ngazi za juu wa vyama vya siasa waliokutana kujadili na kuridhia mapendekezo ya taratibu za uteuzi iliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Kanali mstaafu Lubinga alisema haoni kama kuna tatizo la makundi hayo kupewa nafasi hiyo.

"Kwa nini hawakuwaambia wanajeshi? Kwa  nini hawakuwaambia uhamiaji? Hii ni kwa sababu polisi watatawanywa kusimamia kwenye vituo ambavyo si vyao ndiyo maana wamefanya hivyo," alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa Chadema na Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo, alipopata nafasi ya kuzungumza kwenye warsha hiyo, alionyesha wasiwasi wa kura zitakazopigwa kuwa nani atakayezihesabu.

"Jambo lingine ni kwamba ile siku ya kupiga kura watakuwa huru, hivyo kwa namna yoyote ile watakuja kutudhibiti. Hili ni tatizo na linatupa hofu wanawake hata wanaume. Haya ndiyo mambo ambayo tunapaswa kuyaangalia kwa kina wanatoa wapi suala hilo, kwamba askari wapige kwanza kura siku moja kabla.”

"Ninaamini semina hii italichukulia suala hili kama ni lenye nguvu ya kuona ni namna gani tunaweza kuliangalia ili nchi yetu iwe na amani tunapoelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu," alisema.

WADAU WALONGA

Wakitoa maoni yao kuhusu kura ya mapema, baadhi ya wasiasa na wanaharakati walisema nchi nyingi duniani zimekuwa na kura inayofanana na hiyo, hivyo iwapo sheria hiyo itatekelezwa vizuri hakutakuwa na tatizo.

Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mipango na Uendeshaji wa ADC, Juma Ali, alisema sheria hiyo si mbaya iwapo itasimamiwa vizuri na itawawezesha askari wanaosimamia uchaguzi kufanya kazi zao kwa ufanisi.

"Zanzibar tuna sheria nyingi na nzuri lakini tatizo linakuja katika utekelezaji wake. Nina imani kuwa sheria hii mpya ya uchaguzi iwapo itatekelezwa kama ilivyokusudiwa, itaepusha mitafaruku na migogoro,” alisema.

Naye mwanaharakati wa masuala ya kijamii, Dadi Kombo Maalim, alisema hakuna haja ya kuwa na kura ya mapema na badala yake waliorodheshwa katika sheria ya uchaguzi kupiga kura hiyo, watengewe muda siku yenyewe ya uchaguzi kufanya hivyo.

Alisema kuwapo kwa kura hiyo ya mapema hakutakuwa na uchaguzi huru na haki kwa kuwa kuwapo kwa sheria hiyo ni kutoheshimu mabadiliko ya 10 ya kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

"Sheria hiyo ya uchaguzi haina tija na mantiki yoyote kwa sababu huwezi kutengeneza sheria kwa kikundi cha watu fulani kwa fursa ya kupiga kura," alisema.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Salum Bimani, alisema hakubaliani na kuwepo kura ya mapema kwa kuwa ni utaratibu ambao umelenga kuvuruga uchaguzi.

Alisema utaratibu huo utasababisha kuingiza wapigakura hewa kwa lengo la kukilinda chama tawala kiendelee kubaki madarakani.

ZEC YAFAFANUA

Kutokana na mjadala huo, ZEC imetoa ufafanuzi huku Mkurugenzi wa Huduma za uchaguzi wa tume hiyo, Idrisa Haji Jecha, akisema kura hiyo itawahusisha askari na watendaji ambao watasimamia uchaguzi na wala si kwa askari wa jeshi lote kama ilivyodhaniwa na baadhi ya wanasiasa.

Akizungumza jana na Nipashe, alisema upigaji kura huo utakuwa na utaratibu maalum kwa askari au watendaji watakaosimamia uchaguzi kutakiwa kuiandikia barua tume hiyo mapema ili kupewa kipande maalum kitakachowatambulisha kupiga kura hiyo.

Kwa mujibu wa Jecha, askari au mtendaji yeyote atakayesimamia uchaguzi atakayeiomba nafasi hiyo, ataruhusiwa kwenda kupiga kura katika kituo alichojiandikisha siku moja kabla ya uchaguzi.

"Hii kura ya mapema naona watu wameielewa vibaya. Haitakuwa na udanganyifu wowote kwa sababu kabla ya uchaguzi kutakuwa na orodha kamili ya watu wote watakaopiga kura ya mapema na majina yao yatawekwa hadharani," alisema Jecha.

Alisema kwa mujibu wa Sheria mpya ya Uchaguzi ya mwaka 2018 kifungu cha (82), tume itaweka utaratibu utakaoruhusu upigaji wa kura wa mapema ambao utafanyika siku moja kabla ya siku ya upigaji kura au siku nyingine yoyote kama itakavyoamuliwa na tume.

Pia alisema kifungu hicho kinaeleza kuwa upigaji kura wa mapema chini ya kifungu kidogo cha (1) utatumika katika uchaguzi mkuu au uchaguzi mdogo wa urais pekee.

Alisema kura hiyo itawahusisha kura watakaotelekeza majukumu ya uchaguzi kama msimamizi wa uchguzi, msaidizi msimamizi wa kituo, askari polisi, mjumbe au mtendaji wa tume.

"Mpigakura ambaye atahusika na kazi za ulinzi na usalama siku ya kupiga kura," alisema Jecha alikinukuu kifungu hicho.

Alisema tume ya uchaguzi itakaa na wadau wa uchaguzi ili kuwapa elimu kuhusiana na sheria hiyo ili nao kwenda kutoa elimu kwa wanachama wao.

Juzi, Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous, alisema lengo la vikosi hivyo na watendaji wa tume kupiga kura siku moja kabla ni kuruhusu makundi hayo kupata haki ya kupiga kura na kutekeleza majukumu yao ipasavyo siku ya uchaguzi.

Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari kuhusu kuandika habari za uchaguzi mkuu, alisema hatua hiyo ya kura ya mapema imetokana na marekebisho ya Sheria Na. 4 ya Tume ya mwaka 2018 ambayo inatoa nafasi kwa makundi hayo.

Alisema marekebisho hayo yamekuja baada ya kubainika makundi hayo hayaitumii haki ya kidemokrasia kupiga kura na kuwachagua viongozi kutokana na kutingwa na majukumu ya kazi katika siku hiyo.

"Marekebisho hayo sasa yatawapa nafasi baadhi ya watendaji waliokabidhiwa majukumu, kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika," alisema.

Habari Kubwa