Mil. 5.2 pekee wamesajili laini kwa alama za vidole

20Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mil. 5.2 pekee wamesajili laini kwa alama za vidole

IKIWA imesalia miezi mitatu kabla ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuzifungia laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, watu milioni 5.2 pekee kati ya milioni 44 wanaomiliki simu ndio waliojisajili.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Frederick Ntobi.

Kutokana na changamoto hiyo, kampuni za mitandao ya simu nchini kwa kushirikiana na TCRA, wamezindua kampeni ya pamoja kwa ajili ya kuhamasisha wateja wao kujisajili kwa alama za vidole kabla ya siku ya mwisho.

Takwimu hizo zilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Frederick Ntobi, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja wa wadau wa mawasiliano wenye lengo la kuhamasisha Watanzania kupata huduma hiyo.

Alisema tarehe ya mwisho iliyotolewa na serikali ni Desemba 31, mwaka huu, lakini hadi Agosti, mwaka huu idadi ya watu waliojisajili kwa kutumia kitambulisho cha taifa ni watu milioni 5.2.

"Kwa sasa usajili huu unaendelea katika maduka yote ya watoa huduma za mawasiliano na mawakala wenye vitambulisho maalum na unatarajia kukamilika Desemba 31, mwaka huu.

"Hadi mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, idadi ya laini zote za simu zilizosajiliwa kwa alama za vidole ilifika 5,222,721 ambayo ni sawa na asilimia 12 ya laini zote za simu zilizotumika Sh. 44,258,637," Ntobi alisema.

Alisema juhudi zinazofanywa na TCRA ni kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha kuwa watumiaji wote wa mawasiliano wanasajili laini za simu kwa mujibu wa sheria.

"Baada ya tarehe 31 Desemba mwaka huu, lakini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa upya kwa alama za vidole hazitaruhusiwa kutumika kwenye mitandao ya simu," Ntobi alisisitiza.

Kwa upande wa watoa huduma za simu, walisema changamoto ya watu kutojisajili inatoka na mfumo wa utoaji vitambulisho wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kufanya kazi taratibu.

Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Zantel, Rukia Mtingwa, alisema watu wengi hawajajiandikisha kupata vitambulisho vya taifa ndio sababu wanashindwa kusajili laini zao.

Naye Mwenyekiti wa watoa huduma za mawasiliano ya simu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Alex Bitekeye, alisema wameamua kushirikiana kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael, alishauri watumiaji wote wa simu kujitokeza kujiandikisha na kupiga namba *150*00# chagua namba 3, chagua namba 2, kuingiza majina matatu na nambari ya simu kama yalivyosajiliwa Nida kwa ajili ya kupata namba ya kitambulisho itakayowezesha kujisajili.

Aprili 26, mwaka huu, Rais John Magufuli, alipendekeza muda wa kusajili laini kwa alama za vidole usogezwe mbele kutoka Agosti hadi Desemba 31, ili kutoa fursa kwa Watanzania wengi kuendelea kujisajili.