Stars: Tumekamilika

21Sep 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stars: Tumekamilika
  • ***Yaahidi kuendelea kuwapa furaha Watanzania ikiwafunga Wasudan...

NYOTA na viongozi wa benchi la ufundi la Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), wamesema wako tayari na kamili kuivaa Sudan katika mechi ya kuwania kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)-

-itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda, alisema kuwa kikosi chao kimekamilika na kiko imara kwa ajili wa kuwakabili Sudan na hatimaye kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya kimataifa.

Mgunda alisema kila mchezaji aliyepata nafasi ya kuwa katika kikosi hicho, anafahamu deni na kiu ya ushindi waliyonayo mashabiki na wadau wa soka nchini.

Kocha huyo aliongeza kuwa wataivaa Sudan kwa umakini na tahadhari, kwa sababu nao watakuwa na malengo ya kupata ushindi katika mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 1:00 usiku.

"Tuko kamili, tumefanya mazoezi yetu na kutekeleza kikamilifu programu tulizoziandaa kuelekea mchezo wetu dhidi ya Sudan, kila mchezaji anajua umuhimu wa kushinda vita iliyoko mbele yetu," Mgunda, ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Coastal Union alisema.

Naye Kocha Msaidizi namba mbili wa timu hiyo, Suleiman Matola, aliliambia gazeti hili kuwa wamejiandaa kuwapa Watanzania furaha na si jambo lingine.

“Kila mmoja, kuanzia sisi walimu, tunatambua kuwa mashabiki na Watanzania wote wanataka kuona tunapata ushindi, tena ushindi usiokuwa na shaka ili kazi iwe nyepesi katika mechi ya ugenini, hii inamfanya kila mmoja ajipange kupambana ili kutimiza malengo ya timu na nchi," alisema Matola, nahodha wa zamani wa Simba na Kocha Mkuu wa timu ya Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Kipa mkongwe, Juma Kaseja, amesema kuwa anatamani kupata nafasi ya kucheza fainali za mashindano ya CAF akiwa na Stars na hivyo, amejipanga kuonyesha kiwango cha juu ili atimize ndoto zake.

"Bahati nzuri nimecheza Timu ya Taifa kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 10, lakini sijawahi kucheza fainali zozote zaidi ya Cecafa, wakati Tanzania inafuzu kucheza CHAN kule Ivory Coast sikuwapo, na juzi timu ilipokuwa inatoka AFCON sijakuwepo, natamani siku moja nami nicheze fainali za mashindano yoyote nikiwa na Stars," alisema Kaseja.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Hamasa ya Taifa Stars, Haji Manara, aliwataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kuishangilia timu hiyo ili iweze kufanya vema katika mchezo huo muhimu kwa Watanzania.

Manara alisema kuwa endapo mashabiki wanavyojitokeza kwa wingi, kunasaidia kuwaongezea morari wachezaji na kujiona wana deni kwa nchi yao.

Stars ambayo iliwahi kushiriki fainali za kwanza za CHAN zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2008 ikiwa chini ya Mbrazil Marcio Maximo, ilisonga mbele katika mashindano hayo, baada ya kuwafunga Kenya (Harambee Stars).

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana kati ya Oktoba 18 na 20 mwaka huu wakati fainali za michuano hiyo ya CHAN zimepangwa kufanyika Cameroon hapo mwakani.

Habari Kubwa