Simba yaendelea kujiimarisha Bara

21Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba yaendelea kujiimarisha Bara

ILI kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji inazidi kufanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba, wameifunga Azam B mabao 3-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Mbrazil Wilker da Silva.

Mbrazil Wilker da Silva, ambaye amerejea kwenye timu baada ya kupona majeraha, aliifungia Simba bao la kwanza katika mchezo huo ambao ni sehemu ya mazoezi ya kukijenga kikosi cha mabingwa hao watetezi.

Mabao mengine katika mchezo huo yalifungwa na Kennedy Juma aliyetua Simba akitokea Singida United na kiungo wa Timu ya Taifa ya Sudan, Sharaf Eldin Shiboub.

Simba ambayo ilitolewa katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na UD Songo katika hatua ya awali, inajiandaa na mechi mbili za mikoa ya Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa Septemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na baadaye Septemba 29 mwaka huu, itawafuata Biashara United mjini Musoma, Mara.

Mabingwa hao watetezi wa Bara wana pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili za kwanza msimu huu, walizocheza dhidi ya JKT Tanzania na Mtibwa Sugar.

Habari Kubwa