Lowassa: Nchi sasa imeshika adabu

21Sep 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Lowassa: Nchi sasa imeshika adabu

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amempongeza Rais John Magufuli kwa kurudisha nidhamu kwenye ofisi za umma, akisema sasa nchi imeshika adabu.

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Alitoa pongezi hizo jana wilayani Monduli alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya kwanza ya darasa la saba ya Shule ya Msingi Meyer's inayomilikiwa na Shirika la Mtakatifu Anna.

Lowassa alisema serikali ya awamu ya tano inafanya mambo makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo sekta ya elimu ambayo Rais Magufuli na serikali yake wameamua itolewe bila malipo kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne.

"Nchi imeshika adabu na mambo yanaenda sawa sawa kwa kuwa kila mtu anatekeleza wajibu wake, tofauti na zamani kabla ya nchi haijaingia katika kampeni ya tumbua tumbua, watu walikuwa wanapeleka nchi watakavyo," alisema.

Hata hivyo, Lowassa aliishauri serikali kuelekea nguvu kubwa katika kuboresha elimu ili kuwapa ujuzi wahitimu ili iwe rahisi kwao kujiajiri.

"Kazi kubwa na nzuri anayofanya Rais ya kutoa elimu bure inahitaji kupakwa poda kwani imewawezesha vijana wa sekondari na msingi kumaliza elimu kwa wingi, hivyo tujikite kuwawezesha vijana wetu katika kupata elimu yenye ujuzi ili wajiajiri wanapohitimu," alisema.

Lowasa alisema alishiriki kuhakikisha Shirika la Mtakatifu Anna linapata eneo la kujenga shule na kuwapongeza kwa kujenga shule bila mchango wa mtu yeyote na kusomesha watoto zaidi ya 100 kwa gharama nafuu.

Mwalimu Mkuu wa shule ya hiyo, Sista Anjali Thomas, alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 186 na kati yao, 18 wamehitimu darasa la saba mwaka huu.

Alisema shule hiyo licha ya kuwa na mazingira bora ya kufundishia, inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa gari la shule na barabara ya kuingia shuleni kuharibiwa na mifugo na mvua kutokana na ukosefu wa mifereji ya kupitishia maji.

Mfadhili wa shule hiyo, Padri John Laizer, alimpongeza Lowassa kufanikisha kupatikana kwa eneo la shule na yeye alisaidia upatikanaji wa maji kwa kuchangisha zaidi ya Sh. milioni 52 kwa wadau mbalimbali.

Habari Kubwa