Bosi Usalama wa Taifa awa Balozi

21Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bosi Usalama wa Taifa awa Balozi

RAIS John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali huku aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa (TISS), Dk. Modestus Kipilimba akiteuliwa kuwakilisha Tanzania nje ya nchi.

Dk. Modestus Kipilimba.

Wakati Kipilimba akiteuliwa kushika wadhifa huo, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe na nafasi yake kuchukuliwa na Lootha Sanare, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ilisema Dk. Kipilimba pamoja na mabalozi wengine wateule 11 watapangiwa vituo ambavyo viko wazi kutokana na waliokuwa katika nafasi hizo kustaafu kwa mujibu wa utumishi wa umma au kumaliza muda wao.

Katika uteuzi huo, Rais amemteua Mussa Masele kuwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro. Kabla ya uteuzi huo, Masele alikuwa Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Pia taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli amefanya uhamisho wa wakuu wa wilaya wawili. Katika uhamisho huo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Kabeho anakwenda Chato na Mhandisi Mtemi Msafiri Simione amehamishiwa Wilaya ya Tarime

MAKATIBU WAKUU

Rais amemteua Tixon Nzunda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Maimuna Tarish ambaye alistaafu utumishi wa umma hivi karibuni. Nzunda kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Pia Mary Maganga aliyekuwa Kamishna wa Bajeti ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayeshughulikia Utawala na Mhandisi Anthony Sanga ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Sanga kabla ya nafasi hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza.

Mwingine ni Dk. Ali Possi ambaye ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na nafasi yake inachukuliwa na Gabriel Malata ambaye alikuwa Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika mabadiliko hayo,  Rais amewahamisha Naibu Makatibu Wakuu wawili ambaye ni  Nicolas Merinye William Mkapa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya  Makazi na Mathias  Kabundugulu kutoka Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenda Ofisi ya Rais (Tamisemi).

KIDATA AREJESHWA

Rais ameteua Alphayo Kidata kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara huku Mhandisi Emmanuel Kalebelo akipelekwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro. Pia Dk. Khatibu Kazungu ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro.

WATEULIWA MABALOZI

Katika uteuzi wa jana, Rais aliwateua mabalozi 12 katika nchi mbalimbali akiwamo Dk. Kipilimba ambaye hivi karibuni alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa (TISS).

Wengine walioteuliwa ni Mohammed Mtonga, Gilly Elibariki Maleko, Dk. Benson  Bana, Meja Jenerali (mstaafu) Anselm Bahati, Profesa D. Mbena, Maimuna Tarishi, Meja Jenerali (mstaafu) Gaudence Milanzi, Ali Jabir Mwadini, Justus Nyamanga, Prof. Kennedy Gaston na Mhandisi Aisha Amour.

Sambamba na mabalozi wateule hao, Rais amewapandisha vyeo na kuwateua maofisa watatu kuwa mabalozi. Waliopandishwa ni Steven Mbundi, Ali Sakila Bujiku na Dk. Mussa Lulandala.

Balozi Kijazi alisema wateule hao wataapishwa kesho Ikulu, jijini Dar es Salaam. 

Habari Kubwa