Waziri: JPM ametupatia maelekezo ‘jimbo la Lissu’

23Sep 2019
Augusta Njoji
IKUNGI
Nipashe
Waziri: JPM ametupatia maelekezo ‘jimbo la Lissu’

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amedai wizara hiyo imepewa maelekezo maalum na Rais John Magufuli kuhakikisha inatatua tatizo la maji Jimbo la Singida Mashariki kutokana na wananchi hao kukabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Jimbo hilo ambalo lilikuwa likiongozwa na Tundu Lissu wananchi wake kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na tatizo hilo.

Kufuatia maelekezo hayo, ameagiza wataalamu wa maji kupiga kambi katika jimbo hilo ili kuhakikisha tatizo la maji linakuwa historia.

Aweso alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kumpokea Mbunge mpya wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu.

Alisema Rais Magufuli ameshatoa Sh. bilioni mbili kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.

“Wana Ikungi tuna taarifa zenu miaka tisa mliyokuwa upande wa pili (upinzani) mlikuwa na mateso makubwa sana, Mbunge huyo wa sasa baada ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza aliniuliza mimi suala la maji hakika Waswahili wanasema anayelala na mgonjwa ndiyo anayejua mihemo ya mgonjwa.

“Nimepewa salamu na maelekezo maalum na Rais John Magufuli kwamba nenda Ikungi kawaambie wana-Ikungi serikali itahakikisha inatatua changamoto zinazowakabili na sisi kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha wana Ikungi wanapata maji, tumepewa agizo maalum na Rais, sisi Wizara ya Maji kuhakikisha tunakuja kutatua tatizo la maji Singida Mashariki,” alisema.

Aliongeza: “Kama Mheshimiwa Rais wetu ameshasema, sisi ni nani tusitekeleze agizo lake, maeneo mengi yana shida ya maji, lakini sisi kama wizara lazima tuisaidie Singida Mashariki.”

Aliwaagiza wataalamu hao kubaki Ikungi ili kuanza hatua za awali za kumaliza tatizo hilo.

“Jumatatu (leo) mkakae ofisini tuwape fedha mtekeleze miradi ya maji hapa. Leo nimekuja na timu ya Mkurugenzi Ruwasa tunataka Ruwasa ianze kazi hapa Ikungi mara moja, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa wananchi wa Ikungi kupata majisafi na salama na yenye kuwatosheleza,” alisema.

Alisema wananchi wa jimbo hilo hawataki maneno, wanachohitaji ni huduma ya maji.

Aweso alisema tayari kuna mradi wa maji umekamilika katika kijiji cha Mkiwa na maeneo mengine wataendelea kuchimba visima na kutandika miundombinu ya maji ili wananchi wapate maji ya uhakika.

“Rais ametupa jukumu sisi Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wanapata maji na wasipopata maji atatutumbua, mimi sipo tayari kutumbuliwa….wataalamu wangu tumekuja hapa Isuna kuhakikisha wananchi wanapata maji, mkizingua mimi kijana bwana tutazinguana,” alisema.

Aliwaeleza wananchi hao kuwa wamepata mbunge mzuri sana kwa kuwa si mbunge wa matusi bali ni wa maendeleo.

“Kuna wabunge aina mbili wa matusi na maendeleo, niwaambie tu mmepata mbunge wa maendeleo kwa kuwa anayelala na mgonjwa ndio anayejua mihemo ya mgonjwa, najua wapo watu watakaosema na kukupinga wewe piga kazi, watu hawa ‘wamemiss’ maendeleo wewe ndio wa kuwaletea maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake, Mtaturu alishukuru serikali kwa jitihada zake za kutatua changamoto ya maji katika jimbo lake, ambalo linawakabili wananchi kwa kipindi kirefu sasa ambapo asilimia 41 tu ya Wilaya ya Ikungi ndio inayopata huduma ya majisafi na salama.

Habari Kubwa