Dola mil. 500 kukamilisha maji miji 28

23Sep 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Dola mil. 500 kukamilisha maji miji 28

WIZARA ya Maji imepanga kutumia Dola za Marekani milioni 500 katika miji 28 ili kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji nchini ifikapo 2020.

Sambamba na hilo, imefanya mazungumzo na Serikali ya Poland kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Jumaa Aweso, alisema kiasi hiko cha fedha kimelenga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wanatekeleza kauli ya ‘kumtua ndoo mama kichwani’ ndio maana inaweka jitihada katika suala zima la utatuzi wa kero za maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

"Tuna miradi 483 ya maji ambayo inatekelezwa tuna imani yote itakamilika kutokana na jitihada zinazofanywa na serikali katika sekta ya maji," alisema Aweso.

Alisema serikali haiko tayari kuona upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali ambapo alisema wamekuwa na jitihada za kukutana na wadau  kusaidia kutatua changamoto hizo.

Alisema moja ya mipango thabiti ya serikali ni kuhakikisha inafikisha huduma ya maji vijijini na mijini kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbalimbali ifikapo 2020.

Alisema zipo hatua mbalimbali zinachukuliwa katika utekelezaji huo kwenye miradi ambayo ipo na inaendelea kutekelezwa.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma (DUWASA), Mhandisi David Pallangyo, alisema pamoja na mipango mikakati ya kutatua kero za maji wamepanga kuchimba visima katika baadhi ya maeneo jijini hapa ili kurahisisha upatikanaji wa maji.

Habari Kubwa