Foleni bandarini inavyokosesha mapato serikali

23Sep 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Foleni bandarini inavyokosesha mapato serikali

CHAMA cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo (Tatoa), kimesema foleni ya malori bandarini na mipakani ni changamoto inayoikabili sekta hiyo na kuwafanya washindwe kuhudumia vyema soko la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).

Mwenyekiti wa Tatoa, Angelina Ngalula.

Mwenyekiti wa Tatoa, Angelina Ngalula, aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam, mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho.

Alisema serikali imefungua milango katika soko la Sadc, lakini changamoto kubwa inayosababisha wasafirishaji kuchelewesha mizigo ni foleni zinazosababishwa na taasisi zinazoruhusu mizigo kutoka bandarini kushindwa kufanya kazi kwa umoja.

"Sekta ya usafirishaji imefikiwa kwa asilimia 25 tu na asilimia 75 bado hatujaweza kuhudumia kwa sababu ya kuwapo kwa foleni ya kutoa mizigo bandarini inayosababisha kuchukua hadi saa nane kufika umbali wa kilometa mbili na foleni katika maeneo ya mipaka kama Tunduma," Ngalula alisema.

Kutokana na changamoto hiyo, alisema kwa mwaka wanasafirisha mizigo tani milioni 5.1 wakati mahitaji ni tani milioni 20.

Changamoto hiyo ingetatuliwa wangeshika nafasi ya kwanza kwa kuiingizia serikali fedha za kigeni kutoka nafasi ya pili wanayoshikilia sasa.

Mwaka 2017 waliingizia serikali Dola za Marekani bilioni 1.14 na mwaka 2018 ziliongezeka na kufika Dola bilioni 1.20.

"Mambo tunayojiuliza ni soko lililopo, fursa zilizopo, vikwazo vilivyopo, mapendekezo yetu na mambo yatakayotatuliwa yatasaidia vipi kupambana kuishinda sekta ya utalii inayoongoza kwa kuiingizia serikali fedha za kigeni," alisema.

Aliwashauri wakuu wa taasisi zinazohudumia magari ya kusafirisha mizigo kukutana mara kwa mara ili kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

"Taasisi nyingine katika nchi za wenzetu wanakutana kila Ijumaa, lakini kwetu hapa hawakutani na wanapokutana wanaenda wawakilishi ambao hawawezi kutoa uamuzi na ndio sababu changamoto hazipatiwi ufumbuzi," Ngalula alisema.

Aliiomba serikali kuunganisha tozo zote zinazohusisha magari ya kusafirisha mizigo ili kuondoa usumbufu kwa madereva kuchelewesha mizigo ya wateja.

Waziri Kamwelwe kwa upande wake, alisema wanakutana na Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mipango kwa ajili ya kujadili kwa pamoja kuhusu utoaji mizigo bandarini na kumaliza changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Alisema pia serikali ilishatoa maagizo kuwa, wadau wote wanatakiwa wakae ofisi moja kwa ajili ya kufanya kazi kwa pamoja na kuondokana na changamoto zote za foleni za mizigo bandarini.

 

"Watendaji wote wakae jengo moja, kama mmoja akikwama wajue wanamsaidiaje na ifahamike ni ofisi gani imekwamisha mzigo kutoka bandarini na ikiwezekana apige simu makao makuu ya ofisi yao aseme kuwa amekwama na kama ni shida ya mtandao wautekenye huko ukae sawa," Kamwale alisema.

Aliwataka wamiliki wa malori, kununua mabehewa na vichwa vya treni ili Tatoa nao waweze kuhudumia sekta ya usafiri wa reli wakati ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ukiendelea.

"Tunataka reli ya Tazara ibebe tani milioni tano kwa mwaka na zinazobebwa kwa sasa siwezi kuzitamka. Naomba nyie Tatoa nanyi msimiliki tu malori mnunue na mabehewa na vichwa vya treni ili sasa nanyi msafirishe mizigo kwa njia ya reli," Kamwelwe alisema.

Kuhusu tozo, alisema sekta ya usafirishaji zipo zaidi ya 40 ambazo zote ameshaziainisha kwa ajili ya kuzifanyia kazi na watatoa maamuzi hivi karibuni.

Habari Kubwa