HELSB kuwapa mikopo shule binafsi

23Sep 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
HELSB kuwapa mikopo shule binafsi

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema wanafunzi waliokuwa wanasoma shule binafsi kwa udhamini wa wadau mbalimbali watapewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako

Pia amewataka wanafunzi ambao walishajaza fomu za kuomba mikopo, lakini wakasahau kuweka taarifa zao za ufadhili, wawasiliane na Bodi kwa ajili ya kufanya marekebisho ili waweze kunufaika na fursa hiyo.

Prof. Ndalichako aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua wiki ya elimu na kituo cha kulelea watoto wenye uhitaji katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kimara.

Alisema imejengeka dhana kuwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi hawana uhitaji wa kupata mikopo jambo ambalo si sahihi kwa sababu wapo ambao wanasomeshwa na watu binafsi au wadhamini kama kanisa.

"Naomba niwahakikishie kuwa serikali inatambua watoto hawa ambao wanasomeshwa katika shule binafsi hivyo wanapojiunga na elimu ya juu watapatiwa mikopo, lakini wanatakiwa kuzingatia kujaza maelezo yao vizuri kwenye fomu ya mikopo.

Alisema kama wapo walioshindwa kujaza vyema maelezo yao, Bodi bado inaendelea na usajili hivyo ni muhimu wakaenda kuomba kufanya marekebisho kwa kujaza taarifa hizo kwa usahihi ili waweze kunufaika na mikopo," Prof. Ndalichako alisema.

Alisema serikali inashirikiana na wadau wa sekta binafsi kukuza sekta ya elimu nchini na kwamba wanafanyia kazi changamoto zote.

Awali uongozi wa KKKT Dayosisi wa Mashariki na Pwani, uliiomba serikali iwasaidie kuwapatia walimu na vifaa vya maabara katika shule za kanisa kwa sababu asilimia kubwa ya wanafunzi wanaosoma ni watoto wenye uhitaji.

Habari Kubwa