Aanza kutangaza vivutio vya Same

23Sep 2019
Mary Mosha
SAME
Nipashe
Aanza kutangaza vivutio vya Same

MFANYABIASHARA wa sekta ya usafirishaji mkoani Kilimanjaro, Hussein Abdallah maarufu kama Kilenga, ameanza kazi maalum ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya Wilaya ya Same.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki.

Wilaya hiyo ina vivutio adimu vya utalii katika kilele cha Msitu wa Hifadhi wa Shengena, vivutio vya asili na maisha halisi ya ndege aina ya tai na faru weusi ambao hawapatikani katika mbuga nyingine za Tanzania wanaoishi katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Akieleza nia yake ya kutangaza vivutio hivyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, mfanyabiashara huyo alisema ameanzisha mkakati maalum wa kutangaza fursa zilizopo wilayani humo kwa kutumia mikanda ya video.

“Dhumuni kubwa la kuanzisha kikundi changu cha Lukungu Sanaa Group ni kuhakikisha naitangaza vyema Wilaya ya Same pamoja na vivutio mbalimbali vilivyopo, kuelimisha, kuburudisha, uhamasishaji utunzaji mazingira na kuuenzi utamaduni wa kabila la Kipare.

''Kikundi hiki kilianzishwa mwaka 2017 na baadaye kusajiliwa na Baraza la Sanaa (BASATA) kikiwa na wanachama 15 waliokuwa wakishirikiana katika masuala ya kimuziki na kwa sasa kina albamu mbili, ya kwanza ilitoka 2018 ikiwa na nyimbo 10 na albamu ya pili iliyozinduliwa ina nyimbo 12 zinazoitangaza Wilaya ya Same kiutamaduni pamoja vivutio vyake,” alisema Kilenga.

Waziri Kairuki alisema serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi hao kutangaza vivutio vya asili vilivyopo wilayani humo.

''Nimezisikia changamoto zenu, nimezichukua nitaenda kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na Waziri mwenzangu Dk. Harrison Mwakyembe ili tuone namna gani tunaweza kuwakuza zaidi ya hapa, kwa kuwa mmeonyesha bidii ya kutangaza vivutio vya nchi yetu,” alisema Waziri Kairuki.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya hiyo, Rosemary Senyamule, alitangaza kuwa ofisi yake itaitisha kongamano la wadau wa utalii, kujadili namna bora ya kuchochea hamasa itakayovutia wageni kutoka nchi mbalimbali duniani kuitembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na Msitu wa Hifadhi wa Shengena.

Habari Kubwa