Zahera, Ndayiragije kama wamefanya hivi, ushindi upo

28Sep 2019
Focas Nicas
Nipashe
Zahera, Ndayiragije kama wamefanya hivi, ushindi upo

LEO ni mtindo wa "Kupindua Meza Kibabe" pale wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Yanga, Azam FC na Malindi FC ya Zanzibar watakaposhuka dimbani nchini Zambia, Zimbabwe na Misri kupeperusha bendera ya nchi.

Yanga inayoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itashuka katika Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia kuvaana na Zesco.

Wakati huo Azam ikibeba jukumu la kuhakikisha bendera ya Tanzania inapepea vema kwenye Kombe la Shirikisho Afrika itakaposhuka dimbani Bulawayo, Zimbabwe kuivaa Triangle FC kama ilivyo kwa Malindi FC ambayo itakuwa na jukumu zito la kulipa kipigo cha mabao 4-1 ilichokipata kwenye dimba la Amaan dhidi ya Al Masry ya Misri.

Kwa upande wa Yanga inahitaji ushindi wowote ama sare ya zaidi ya bao moja ili kuweza kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo kutokana na mechi ya awali Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Lakini kwa Azam yenyewe inapaswa kushinda ili kuweza kusonga mbele kufuatia mechi ya awali katika Uwanja wake wa Chamazi kukubali kipigo cha bao 1-0.

Ninaamini kwa maandalizi yaliyofanywa na wawakilishi wetu hao kupindua matokeo ugenini ni jambo linalowezekana pasi na shaka.

Jeuri ya matumaini hayo ninaipata si tu kwa sababu ya maandalizi bali pia ujasiri na rekodi ya timu hizo na makocha wao kushinda ugenini.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba Yanga iliweza kupindua matokeo ugenini Botswana kwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Township Rollers baada ya sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa raundi ya awali ya michuano hiyo.

Hivyo, ni wazi itashuka dimbani leo ikiwa inajiamini na ujasiri mwingi wa kuweza kupindua matokeo kutokana na rekodi yao hiyo.

Aidha, kwa upande wa Azam kikubwa ninafahamu rekodi nzuri ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije aliyeiwezesha timu ya Taifa, Taifa Stars kupindua matokeo ugenini dhidi ya Kenya, Harambee Stars.

Wakati huu Ndayiragije akikaimu nafasi ya Kocha Mkuu wa Stars, alikiwezesha kikosi hicho kutinga raundi inayofuata ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), kwa kuitoa Harambee Stars kwao kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya sare tasa nyumbani na ugenini.

Lakini pia ikumbukwe kuwa Azam itashuka dimbani ikiwa inajua haina cha kupoteza jambo ambalo litawafanya kuongozwa na falsafa ya kushambulia zaidi hivyo presha kubwa kuwa kwa wenyeji watakaokuwa wakitaka kulinda ushindi wao wa awali.

Si hivyo tu, bali pia makocha wa timu hizo, Mwinyi Zahera wa Yanga na Ndayiragije wote wameshawasoma wapinzani wao na wanajua nini cha kufanya ili kuweza kuibuka na ushindi leo.

Kikubwa zaidi ninachokitarajia kukiona kama Zahera na Ndayiragije wamewaandaa wachezaji wao kufanya kushambulia mwanzo mwisho ili kuwafanya wapinzani wao kujilinda zaidi na kutoruhusu kushambuliwa, ushindi lazima upatikane.

Lakini pia hilo litawezekana tu kama Zahera na Ndayiragije watakuwa wamewaelekeza wachezaji wao hususan mabeki na viungo kukabia dimba la kati, lakini pia wakicheza kitimu zaidi kwa kuzuia na kushambulia.

Ninaamini makocha wameyafanyia kazi hayo na kilichobaki ni wachezaji kutekeleza majukumu yao uwanjani, hivyo kinachotakiwa kwa wadau wa soka na Watanzania wote niĀ  kuwaombea wawakilishi wetu hao na kuwatakia kila la kheri kupata ushindi leo ili bendera ya Tanzania iendelee kupepea katika michuano hiyo ya ngazi ya juu kwa klabu barani Afrika.

Habari Kubwa