TFF imtangaze kocha Stars kuokoa balaa hili

30Sep 2019
Mhariri
Nipashe
TFF imtangaze kocha Stars kuokoa balaa hili

KWA muda sasa Kocha Mkuu wa Azam FC, Etienne Ndayiragije, amekuwa akikaimu nafasi ya kocha mkuu wa Taifa Stars, tangu Mnigeria Emmanuel Amunike alipotimuliwa mapema Julai mwaka huu.

Katika majukumu hayo ya kuinoa Stars, Ndayiragije amekuwa akisaidiwa na Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Suleimani Matola pamoja na Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda.

Kwa ujumla kocha mkuu wa timu yoyote ya taifa ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo, hana budi kuwa huru katika kazi hiyo, huku akipata nafasi ya kutosha kuzunguka huku na kule katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu husika ili kuweza kutazama viwango na uwezo wa wachezaji mbalimbali watakaounda kikosi chake.

Si katika Ligi Kuu husika tu, bali pia kwenye ligi mbalimbali zinazoendelea nchini na hata nje ya nchi ambako kuna wachezaji wazawa wanaocheza huko pindi anapotaka kujiridhisha zaidi na viwango vyao kabla ya kuwajumuisha kikosini.

Lakini kwa Ndayiragije na wasaidizi wake wote ni wazi wamekuwa wakibanwa na majukumu ya waajiri wao, klabuni, hivyo kukosa muda wa kutosha kuzunguka huku na kule kutazama uwezo wa wachezaji kabla ya kuwaita Taifa Stars.

Ndiyo sababu wachezaji wanaoitwa Taifa Stars, wengi ni waliowahi kupita mikononi mwa Matola, Ndayiragije na Mgunda au walioko katika klabu wanazozifundisha ama wale waliokuwamo timu ya taifa kwa muda mrefu.

Mfano mzuri ni wakati huu ambao Ligi Kuu Bara ikiendelea tulitarajia kumuona Ndayiragije amegawana majukumu na wasaidizi wake Matola na Mgunda kwenda kushuhudia mechi mbalimbali za ligi hiyo ama hata kwenda kuona namna wachezaji wao walioko Yanga walivyocheza dhidi ya Zesco kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini Ndayiragije alikuwa bize katika kuiongoza Azam dhidi ya Triangle FC nchini Zimbabwe kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, huku Matola na Mgunda wakipambana kuziongoza Polisi Tanzania na Coastal Union kwenye mechi zao za Ligi Kuu.

Kwa utaratibu huo, kuelekea mechi ijayo ya marudiano ya Taifa Stars dhidi ya Sudan kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), Ndayiragije atajuaje kama uwezo wa mchezaji wa Simba ama Yanga walioko Stars umepanda ama umeshuka? Ni wazi atawaita kwa mazoea tu, lakini pia atakosa nyota wapya wanaoonyesha uwezo dimbani kutoka klabu hizo na nyingine za Ligi Kuu.

Kwa ujumla kazi aliyoifanya Ndayiragije na wasaidizi wake kwa kufanikiwa kwanza kuitoa Kenya kwenye kinyang'anyiro hicho cha kufuzu CHAN kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare tasa nyumbani na ugenini na sasa wakikabiliwa na mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan ugenini baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ni kubwa.

Lakini ikumbukwe Ndayiragije na wasaidizi wake wameiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza hatua ya makundi kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 baada ya kuitoa Burundi. Hivyo, walipoifikia ni mafanikio makubwa na wanapaswa kupongezwa hasa kutokana na majukumu ya kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.

Sote tumeona namna Ndayiragije anavyolemewa na majukumu na kushindwa kuiongoza vema klabu yake, jambo ambalo ni wazi limechangia Azam FC kutolewa Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kwa mfano huo huo tunaona namna Mtibwa Sugar ilivyoanza vibaya msimu huu wa Ligi Kuu, hali hiyo ni wazi imetokana na Kocha Mkuu, Zuberi Katwila kuwa na Kikosi cha timu ya Taifa cha U-20 kwenye michuano ya Cecafa U-20 nchini Uganda.

Nipashe tunaona ni wakati muafaka kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuteua rasmi kocha mkuu wa Stars na Taifa U-20 na kama inaona Ndayiragije na wasaidizi wake pamoja na Katwila wanatosha, basi wakae meza moja na klabu zao ili kukubaliana na kuwaidhinisha rasmi kubeba majukumu hayo ya taifa.

Habari Kubwa