Hili la Mauya kwa Ajibu, refa Mwandembwa anatosha?

30Sep 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Hili la Mauya kwa Ajibu, refa Mwandembwa anatosha?

MOJA ya mambo ambayo hayatosahaulika kwenye Ligi Kuu msimu uliopita ni kitendo cha mchezaji wa Mbao FC, Rafael Siame kuokoa maisha ya mchezaji wa Coastal Union Adeyum Salehe.

Kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Adeyum alianguka mwenyewe uwanjani dakika ya 44 na kung'ata ulimi hali iliyosababisha nusura apoteza maisha.

Siame, aliyekuwa karibu yake, pamoja na kwamba si mchezaji wa timu yake, alimkimbilia haraka na kuingiza kidole mdomoni ili kuurudisha ulimi kwenye hali ya kawaida na kufanikiwa.

Ni jambo ambalo halikuzungumzwa sana, wala Siame kupata tuzo kutoka kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), lakini kilikuwa ni kitendo cha uungwana sana na cha kibinadamu.

Moja kati ya matakwa ya Shirikisho la Soka duniani (FIFA) ni mchezaji kulinda usalama wa mchezaji mwenzake, iwe wa timu yake au timu pinzani na kitendo chochote cha kumsababishia kuhatarisha maisha yake, au kukatisha ndoto yake ya kucheza soka hakikubaliki.

Alhamisi iliyopita kwenye mechi ya Ligi Kuu kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba kulitokea tukio ambalo limekuwa gumzo kubwa sasa sehemu mbalimbali ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii kama kawaida.

Ni cha mchezaji wa Kagera Sugar Zawadi Mauya, kumpiga mateke yapatayo manne kwa makusudi Ibrahim Ajibu.

Ukiangalia tukio hilo utagundua kuwa Mauya hakuwa anacheza rafu, ila alikuwa anampiga mchezaji mwenzake mateke kwa makusudi. Haikujulikana dhamira hasa ya mchezaji huyo.

Marudio yanaonyesha kuwa alimpiga kwanza mateke mawili. Baadaye akampiga la tatu ambalo badala ya Ajibu kuanguka lilimfanya yeye mwenyewe aliyepiga kupepesuka na kutaka kuanguka.

Aliposimama anaenda tena kumpiga teke lingine la nne, ambalo hili ukilitazama kwa jicho la tatu alikuwa na lengo la kumchota mtama kabisa, lakini alifanikiwa kuufyatua mguu mmoja wa Ajibu na mwingine ukabaki, hali iliyosababisha asiweze kuanguka chini.

Wakati Mauya akicheza rafu hizo, Ajibu ndiyo alikuwa na mpira. Na Mauya hakuonekana kabisa kuwa na nia na mpira. Alichotaka yeye ni kumpiga mwenzake mateke ya makusudi.

Rafu za aina ile nilikuwa nikiziona zamani kwenye miaka ya '80 na '90 kwenye mechi za uswahilini. Kwa miaka hii hata huko mchangani huwezi kuzikuta rafu za aina ile.

Cha ajabu na cha kusikitisha, wakati tukio lile likitokea, mwamuzi Emmanuel Mwandembwa alikuwa karibu na tukio. Lakini alichofanya ni kumpa Mauya kadi ya njano tu.

Sijui Mwandembwa alitaka kitu gani zaidi Mauya aongeze ili atoe kadi nyekundu. Kwa waliotazama karibuni wote, wanakiri kuwa ile haikuwa rafu bali ni uhuni uliopitiliza.

Baada ya mashabiki wengi wa soka kulizunguzia tukio hilo baya na lenye kutia najisi soka la Tanzania, huku wengi wakimsakama mchezaji huyo kwenye mitandao ya kijamii, akaamua kuomba radhi kwenye mtandao wake wa kijamii.

"Nachukua nafasi hii kukuomba radhi rafiki, na mchezaji mwenzangu Ibrahim Ajibu kwa mchezo usio kuwa wa kiungwana hapo jana, ni tukio ambalo hutokea ndani ya mchezo ikiwa umefungwa na damu ikiwa imechemka. Na pia niuombe radhi uongozi wangu wa Kagera Suger na Simba pamoja na mashabiki zangu kwa ujumla, asanteni sana."

Napenda kumpongeza mchezaji huyo kwa kutambua kuwa alichofanya ni kosa na wala haikuwa rafu ya kawaida ya mpira. Lakini anapaswa kuwa makini na tabia hiyo kwani itakuja kumharibia katika maisha yake ya soka huko mbele ya safari.

Hakuna timu ambayo inaweza kumsajili mchezaji asiye na nidhamu, kwani anaweza kuigharimu wakati wowote. Wachezaji wote ni ndugu moja kwani wanaweza kukutana siku nyingine kwenye klabu moja.

Mauya anatakiwa aige mfano wa Siame na si alivyofanya. Kuhusu Mwandembwa ni kwamba Kamati ya Waamuzi na ile ya Saa 72 inaweza kufanya kazi yake, lakini naye inapaswa ajiulize kama kweli anatosha kuendelea kuifanya kazi hiyo.

Waamuzi wana dhima ya kwanza kulinda afya ya wachezaji, hivyo wanapoona kuna mchezaji mechi imemshinda na anachotaka ni kuvunja wenzake miguu anatakiwa ampumzishe na si kumlealea.

Inaonekana sasa siyo Ligi Kuu, bali ni mechi za mchangani. Vinginevyo kuna mchezaji siku nyingine anaweza kumvunja mwenzake mguu kwa makusudi akitegemea huruma kutoka kwa refa kama ilivyokuwa kwa Mauya.

Waamuzi kutokuwa makini na kuachia mambo ya kihuni uwanjani, ndiko kunazalisha majeruhi wengi ambao wakati mwingine wanakuja kuigharimu timu ya taifa.

Wakati mchezaji fulani anatakiwa aiwakilishe nchi, anakuwa ni majeruhi ambayo yalisababishwa tu na aina ya mchezaji kama Mauya na refa kumvumilia bila kumwadhibu ipasavyo.

Habari Kubwa