Kamusoko, Lwandamina waeleza waliposhikwa Yanga

30Sep 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kamusoko, Lwandamina waeleza waliposhikwa Yanga

KIUNGO wa Zesco FC ya Zambia, Thabani Kamusoko na Kocha Mkuu wa klabu hiyo, George Lwandamina, wamesema kikosi cha Yanga kimeimarika na kimekuwa imara tofauti na walivyokutana katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, lakini wakieleza walipowashikia-

-wawakilishi hao wa Tanzania kimataifa.

Hata hivyo, Zesco wamesonga mbele katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), baada ya juzi waliporudiana kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola kupata ushindi wa mabao 2-1.

Akizungumza na Nipashe juzi, Kamusoko, alisema Yanga walijaribu kupambana na kufanikiwa kuwadhibiti katika eneo la katikati, lakini mbinu yao ya kushambulia kupitia pembeni iliwasaidia kusawazisha na baadaye kupata bao la kuongoza katika mchezo huo.

Kamusoko alisema Yanga ilikuwa na mipango imara na kama si kutumia uzoefu waliokuwa nao, mchezo huo ungekuwa mgumu zaidi kwa upande wao.

"Yanga walikuja na mipango, walikuwa imara zaidi na wamebadilika tofauti na tulivyokutana nao katika mchezo wa kwanza, walifanikiwa kutudhibiti katikati, tukalazimika kufanya mashabulizi kupitia pembeni na tunashukuru tulipata bao la kuongoza," Kamusoko alisema.

Naye Kocha wa Zesco FC,  Lwandamina, alisema kikosi cha Yanga kimeimarika na kimewasumbua tofauti na walivyotarajia.

"Wameimarika, leo ( juzi), wamecheza vizuri zaidi kuliko walivyokuwa katika mechi ya mkondo wa kwanza, wakiendelea hivi, watafanya vizuri katika ligi na mashindano mengine watakayoshiriki," alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.

Zesco imetinga hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga sasa imehamia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo itacheza mechi moja ya mchujo na ikipata matokeo ya jumla nyumbani na ugenini itatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.