Simba kuanza kujifua uwanja wake wa Bunju

30Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba kuanza kujifua uwanja wake wa Bunju

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatarajia kuanza kutumia uwanja wake wa Bunju kwa ajili ya kufanya mazoezi ili kujiandaa na mechi za ligi hiyo na mashindano mengine mbalimbali watakayoshiriki kuanzia Oktoba mwishoni, imeelezwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed "Mo" Dewji, alisema mchakato wa ujenzi wa uwanja wa nyasi bandia na nyasi halisi unaendelea vizuri na utakamilika mwezi ujao na timu itaanza kuutumia muda si mrefu.

Dewji alisema kuwa ujenzi wa vyumba vya kubadilishia nguo umekamilika na kuufanya mradi huo kwenda na malengo waliyojiwelea mapema mwaka huu.

Leo (juzi), nilitembelea uwanja, maendeleo ni mazuri, uwanja wa nyasi bandia na nyasi halisi uko katika hatua za mwisho, utakamilika Oktoba mwishoni, na mara tu ukikamilika, timu yetu (Simba) itaanza kufanya mazoezi hapa," alisema Dewji.

Baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya uwanja huo, mwekezaji huyo ataendelea na mchakato wa kutengeneza majukwaa kwa ajili ya mashabiki watakaofika kuwaona mabingwa hao.

Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, aliweka jiwe la msingi kwenye uwanja huo.

Habari Kubwa