Simba inajipigia tu

30Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Simba inajipigia tu
  • ***Kagere, Miraji washika usukani wa kuchana nyavu, shuti la Ndemla nusura lizue jambo kwa....

BAADA ya kuvuna pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar Alhamisi iliyopita, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba jana, waliendeleza vipigo katika ligi hiyo baada kuipiga Biashara United kwa mabao 2-0 katika mechi kali iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Mshambuliaji Meddie Kagere ndiye aliyekuwa wa kwanza kuiandikia Simba bao la kwanza katika dakika ya 22 kabla ya Miraji Athumani kutupia la pili kipindi cha pili dakika ya 74.

Kagere ambaye katika mechi dhidi ya Kagera Sugar alifumania nyavu mara mbili wakati wakishinda 3-0, jana alifunga bao hilo akiitendea haki krosi ya Miraji kutoka wingi wa kulia ambaye jana alianza kwa mara ya kwanza msimu huu, baada ya mechi zilizopita Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Patrick Aussems kuwa na utamaduni wa kumchezesha akitokea benchi.

Miraji kwa upande wake alifunga bao la pili kwa kichwa akiunganisha nyavuni mpira wa faulo iliyopigwa na Ibrahimu Ajibu.

Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 12 baada ya kushinda mechi zake zote nne ilizocheza msimu huu na sasa inarejea Dar es Salaam, na huenda ikacheza mechi yake iliyokuwa imeahirishwa dhidi ya KMC kabla ya Kalenda ya Fifa ambayo inaanza Oktoba 7 hadi 19, mwaka huu.

Aidha, Kagere naye ameendelea kukaa kileleni mwa orodha ya wafungaji bora akiwa na mabao sita, huku Miraji akifuata kwa kucheka na nyavu mara tatu.

Hata hivyo, baada ya kalenda hiyo ya Fifa, inaonyesha Simba itakutana dhidi ya Azam FC Oktoba 23 na kisha siku tatu baadaye kuifuata Singida United kabla ya Oktoba 30, mwaka huu kwenda Shinyanga kuivaa Mwadui FC.

Katika mechi ya jana, Simba ambayo ilimiliki mpira mwanzo mwisho, kama ingekuwa makini ingeweza kupata mabao mengi zaidi kwani Kagere alishindwa kuiandikia timu yake bao la pili dakika ya 29 akiwa amebaki na kipa kabla ya Hamisi Ndemla dakika ya 40 kushindwa kuwa makini kwa kumhadaa mlinda mlango wa Biashara United na badala yake akaachia shuti kali lililoishia kifuani kwa kipa ayepata maumivu na kuhitaji kupatiwa huduma ya kwanza.

Biashara United ilikuwa ya kwanza kufanya mabadiliko katika dakika ya 51 kwa kumtoa Victor Hangaya na nafasi yake kuchuliwa na Jerome Lembele kabla ya dakika ya 72 Simba kumtoa Hassan Dilunga na kumwingiza Francis Kahata, huku dakika moja baadaye Mussa Khamis akimpisha Ramadhan Chombo kwa upande wa 'Wafanyabiashara' hao wa Musoma.

Dakika ya 77 Kocha wa Simba, Aussems alifanya mabadiliko kwa Ajibu kumpisha Sharaf Shiboub na dakika sita baadaye Miraji akitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Deo Kanda.