Ipokeeni tena fursa hii ya kusamehewa

01Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Ipokeeni tena fursa hii ya kusamehewa

TUNAMPONGEZA Rais John Magufuli, kwa kupendekeza utaratibu wa washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi kukiri makosa, kuomba msamaha na kurudisha fedha na mali wanazomiliki, wakiamini kuwa zina walakini.

Tunaipongeza hatua ya Rais ya kuwa kiongozi pekee aliyeibua utaratibu huo, hapa nchini na kuanza kutekeleza jukumu hilo ambalo tunaona kuwa lina tija kwa nchi na wahusika.

Kadhalika, tunawapongeza wahusika takribani  460 walioitikia wito wa kuomba msamaha na kuahidi kurudisha fedha hizo na kukubali kusamehewa na Rais.

Aidha, tunaungana na maelezo ya Rais kuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), imefanya kazi kubwa ya kuwapokea, kuwasiliana na wahusika kuwasikiliza na kupitia nyaraka zao na kwa moyo wameamua kuomba msamaha na kurejesha kile walichoamini kuwa kilistahili kuwa mikononi mwa  serikali.

Tumpongeza Rais kuonyesha moyo wa upendo, huruma na kuthamini utu wa watu hao, ambao hata kama pengine walikuwa na hofu kuwa wametegwa amewaahidi kuwa amewasamehe na hiyo ni kweli na ni haki yao.

Ikumbukwe kuwa kuwasamehe wahusika  kunamaanisha mambo mengi si kwa mshtakiwa mwenyewe lakini pia, familia yake na taifa ambalo lilikuwa linawahudumia wakiwa mahabusu magerezani.

Wale ambao bado wanatafakari wakumbuke kuwa msamaha huo ni dawa kwao hasa kwa kuwa wamekaa muda mwingi gerezani na baada ya kuendelea kujichunguza na kuona kuwa wana stahili kuungama wafanye hivyo.

Tunaomba umma ufahamu kuwa kuingia gerezani ama kufikishwa mahakamani si jambo la mtu mmoja kila binadamu ana hatia ambayo inaweza kumfikisha mahakamani pamoja na jela.

Ni vizuri familia na jamaa za wahusika zikawashauri kwa weledi kama kuna uwezekano wa kunufaika na msamaha huo wafanye hivyo wasipoteze wakati.

Tunasema hivi hakuna cha kuhofia kwa sababu  kila mtu ni mfungwa au mshtakiwa mtarajiwa.

Tena tukumbuke kuwa kinachowatofautisha walio uraiani na magerezani ni kwamba ambao hawajashtakiwa ni kwa sababu hawajakamatwa kutokana na hatia zao, lakini nao pia wana sababu na sifa zote za kuwafanya kufikishwa mahakamani na magerezani.

Wahusika wakumbuke kuwa kupata msamaha baada ya kuomba radhi na kurejesha mali pamoja na kuondoka  gerezani ni jambo la kuwafariji na kuwapa ushujaa wa kukiri kuwa walikosea na wakaomba msamaha  ili wakaanze upya maisha yao.

Tunawashauri wahusika wajitie moyo wa ushujaa na kuachana na mambo ya zamani wakumbuke kuwa kupata msamaha nako ni fursa ya kujenga upya kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Wafahamu  kuwa kila binadamu anapitia kwenye mambo mengi ambayo yanamkuza kutoka hatua moja kwenda jingine na hilo wanalolipitia ni kama darasa.

Waombe radhi na waichukulie hali hiyo  kuwa  ni nafasi nyingine ya kujifunza kuhusu harakati za maisha, kujikwaa, kuanguka lakini pia kusimama tena.

Wahusika wafahamu kuwa nia ya serikali ni njema na imelenga pia watu wengine wajifunze na wawe tayari kubadilisha mienendo yao hasa katika uadilifu na ulinzi wa mali za umma.

Tunaamini kuwa msamaha wa Rais hautapita na kusahaulika bali utaacha alama za kujitizama upya kama taifa, kubadilika na kutumia fursa hiyo kama njia ya kutafakari njia na mienendo yetu.

Tafakari hiyo si kwa wahusika peke yao ambao wanaweza kuomba msamaha na kurudisha mali za Watanzania  bali ni kwa kila mmoja.

Wengi watakubaliana nasi kuwa kukamatwa, kufikishwa mahakamani na hata kufungwa gerezani ni mambo yanayotokea katika maisha ya binadamu wote.

Tunawahimiza tena kujichunguza na kutumia fursa hiyo kuomba radhi ili kunufaika na msamaha wa Rais.

Habari Kubwa