Siku ya Wazee, halmashauri ziige mfano wa Ubungo

01Oct 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Siku ya Wazee, halmashauri ziige mfano wa Ubungo

OKTOBA Mosi ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wazee katika dhima nzima ya kuangalia ustawi katika umri wao wa uzee, unaombatana kwa sehemu kubwa na changamoto mbalimbali za kimaisha.

Pamoja na zingine kwa ujumla wake, changamoto zinazowakabili wazee ni pamoja  na  kutolipwa kwa wakati mafao yao pindi wanapostaafu.

Vilevile zipo changamoto za ukosefu wa lishe bora na kubwa zaidi kwa minajili ya safu hii leo, suala la kukosa huduma bora za afya na hivyo kuathiri ustawi wao.

Hili si kwa Tanzania tu, bali ni changamoto inayowakumba takribani wazee wote katika maeneo tofauti ya dunia.

Na ndiyo sababu ambayo kimsingi imechangia Umoja wa Mataifa (UN) kupitia majukwaa yake mbalimbali likiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO), kuja na siku hii ya kimataifa ya wazee.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya wazee nchini kwa maana ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi ni milioni 2.5, sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania wote takribani milioni 55 kwa hivi sasa.

Kwa mwaka huu, maadhimisho ya siku hii yanafanyika Manispaa ya Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kauli mbiu ya mwaka huu kwa maadhimisho haya ni ‘Tuimarishe Usawa Kuelekea Maisha ya Uzeeni’ ikikusudia kuihimiza serikali na kwa maana hiyo nchi wanachama wa UN, kuweka mipango na mikakati ya kupunguza tofauti za watu katika jamii.

Si hilo tu, pia kutoa fursa kwa makundi maalumu likiwamo la wazee kufaidika na fursa zilizopo na maendeleo yaliyofikiwa katika nchi husika.

Kimsingi Muungwana anakiri kwamba serikali inaendelea na jitihada za kujenga uelewa kwa jamii juu ya changamoto zinazolikabili kundi hili na hususani katika eneo la kuhakikisha wazee wanapata huduma bora za afya.

Inachukua hatua za kuwabaini wazee wote kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa, kata, wilaya, mkoa hadi ngazi ya taifa.

Aidha, inachukua hatua za kuhamasisha kuundwa kwa mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya kijiji au mtaa, hadi ya taifa, kuwapatia vitambulisho vitakavyowawezesha kupata huduma za matibabu bila ya kulazimika kuzilipia.

Serikali iko pia katika mpango wa kuhakikisha wanapata Bima ya Afya ili waondokane na kero wanazokumbana nazo wanapohitaji huduma za afya.

Pamoja na kwamba hatua hizi chanya bado hazijaenea katika maeneo yote nchini, Muungwana ana ushuhuda wa baadhi ya halmashauri ambazo zimeweza kimsingi kutimiza wajibu wa kuliangalia kundi hili katika eneo la afya.

Mojawapo ya halmashauri hizo ni ya Manispaa ya Ubungo, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Wazee katika manispaa hii walau wanatibiwa bure katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya ambako Muungwana amefanya utafiti wake mdogo.

Kwamba halmashauri hii imeweza kutoa huduma kwa wazee bila ya kuwatoza fedha katika zahanati na vituo vyake vya afya, hatua ambayo ni ya kupigiwa mfano.

Sasa wakati leo dunia inaadhimisha Siku ya Wazee Kimataifa, Muungwana anaona wakati umefika kwa halmashauri zote nchini kuwezesha hili la kutoa huduma bora za afya kwa wazee walio katika maeneo yao bila malipo.

Ninasema hivyo kwa sababu kuna halmashauri ambazo zimeweza kufanya hili kwa ufanisi, kama hiyo ya Ubungo inayotolewa mfano.

Msingi wa msisitizo huo umejikita vilevile katika ukweli kwamba UN imepitisha Azimio la kisiasa kuwahi kufikiwa linalochochea afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus, azimio hilo linahimiza dunia ambamo kwao afya si gharama bali ni uwekezaji.

Dunia ambamo afya inachagiza maendeleo endelevu, ambayo kila mtu wakiwamo wazee atafurahia apaswavyo kuwa nayo.

Habari Kubwa