Waombaji 10,000 HELSB wakutwa na kasoro

01Oct 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Waombaji 10,000 HELSB wakutwa na kasoro

WAOMBAJI 10,452 kati ya 81,992 wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2019/20, wamekutwa na dosari kwenye maombi yao zinazoweza kuwanyima sifa ya kupata mikopo hiyo.

Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa HESLB, Veneranda Malima

Kwa mujibu wa tangazo lilitolewa juzi kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB), waombaji hao wamepewa muda wa siku nne kurekebisha kasoro hizo.

Kwa mujibu wa nyaraka hiyo wengi wa waombaji wana makosa kwenye eneo la vyeti vya kuzaliwa vinavyotolewa na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Nyaraka hiyo imeonyesha zaidi ya waombaji 10,000 wana kasoro kwenye vyeti vya kuzaliwa na wametakiwa kurekebisha kuanzia jana hadi Oktoba 3.

"Hatua ya HESLB inafuatia kukamilika kwa uhakiki wa maombi ya mikopo na kubainika baadhi ya fomu za maombi ya mikopo zina upungufu unaozuia kuendelea na hatua ya kupangiwa mikopo," alisema.

Pia tangazo hilo lilibainisha kuwa upungufu huo ni pamoja na kukosa nyaraka ama viambatanisho vilivyothibitishwa na mamlaka husika na saini za waombaji na wadhamini wao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa HESLB, Veneranda Malima, alisema mwongozo unasema mwanafunzi ataweka viambatanisho ambavyo vimethibitishwa na mamlaka husika.

"Baadhi yao wameweka vyeti, lakini hakikuthibitishwa na hizo mamlaka na kukifanya kisiwe halali, tumetoa siku nne kuthibitisha nyaraka hizo wakishindwa hawataingia kwenye hatua inayofuata ya kugawiwa mikopo," alisema.

Veneranda alisema majina hayo yamebainika wakati wa kupitia orodha ya waombaji na baada ya siku hizo kupita wanaanza kugawa mikopo kwa waombaji wenye sifa.

Aprili mwaka huu, Rita ilitangaza kuanza uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kwa wanafunzi wanaotaka kuomba mikopo kupitia mfumo wa kielektroniki.

Wanafunzi hao walitakiwa kujaza fomu maalum kwenye mtandao na kuambatanisha vyeti vyao ili kuhakikiwa kama walivyonavyo ni sahihi.

Rita ilieleza kuwa baada ya uhakiki, majina ya wahusika yatapelekwa Bodi ya Mikopo kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kupatiwa mikopo kwa mujibu wa sifa zilizoainishwa na bodi hiyo.

Mwaka jana Rita ilifanya uhakiki wa vyeti 108,000 kati yake 2,000 vilibainika kuwa na kasoro mbalimbali ikiwamo kughushi na wapo waliofikishwa mbele ya vyombo vya sheria.