Muswada wa Makonda wamtisha waziri

01Oct 2019
Joseph Mwendapole
Nipashe
Muswada wa Makonda wamtisha waziri

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Agustino Mahiga, amesema baadhi ya wabunge wamemtisha kuwa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mirathi uliowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni kaa la moto.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Agustino Mahiga

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mjadala kuhusu kuelekea mabadiliko katika Sheria ya Kimila na Mirathi ulioandaliwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF).Dk. Mahiga alisema kunahitajika elimu ya kutosha kwa wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na kimila kwa kuwa sehemu kubwa ya muswada huo inagusa imani za watu, hivyo haitakuwa rahisi kufanya mabadiliko bila kuwapa elimu.

“Ninyi WiLDAF na wadau wengine mnapaswa kufanya kazi kubwa sana ya kuelimisha watu kwa sababu kuna wabunge wameshaniita na kuniambia huo muswada uliopewa ni kaa la moto. Sasa hii ni dalili kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya, hivyo kaeni na wadau muwaelimishe umuhimu wa mabadiliko,” alisema Dk. Mahiga.

Pamoja na hayo, Dk. Mahiga alisema serikali itaendelea kutatua changamoto za kimila wanazokutana nazo wajane, wanawake na watoto katika masuala ya mirathi ili kuhakikisha wanapata haki.

Waziri Mahiga alisema kama tatizo ni sheria, serikali iko tayari kupokea maoni ya wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na WiLDAF ili kuwa na sheria itakayotoa haki sawa kwa wote, yaani wanawake, wanaume na watoto.

“Sote tunafahamu kuwa Sheria ya Kimila Na. 4 inatokana na mila na desturi zetu. Ombi langu kwenu mwendelee kuhamasisha jamii kujali familia, wanawake na watoto kwani mabadiliko makubwa yanayotakiwa ni ya kifikra na jamii kuacha kudhulumu mali za marehemu kwani watoto wataathirika,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa WiLDAF, Anne Kulaya, alipongeza serikali kwa kupokea rasimu ya mabadiliko ya sheria ya mirathi waliyoiwasilisha serikalini na kwamba anaamini serikali itaifanyia kazi.

Habari Kubwa