Mbowe abadili mada kuwakwepa polisi

01Oct 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Mbowe abadili mada kuwakwepa polisi

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, jana alilazimika kuendesha mkutano wa ndani huku kamanda wa polisi wa wilaya akiwa ndani na polisi wengine wakiwa wamezingira nje ya jengo.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Kikao hicho ambacho ni cha ndani, kiliongozwa na Mbowe ambaye ni Mbunge wa  Hai. Kutokana na polisi kuingilia mkutano huo, alijikuta akibadilisha mwelekeo wa mazungumzo yake huku akiwasifia polisi kwa kuhudhuria mkutano huo pia akiwapiga vijembe kiaina.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, Mbowe alisema anashangazwa na woga uliopo licha ya vyama vya upinzani kutoruhusiwa kufanya mikutano.

"Mnaogopa nini? Ushindani? Mmefunga wenzenu mikono miaka minne, mmewafunga miguu miaka minne, ngoma (uchaguzi) unanyanyuka keshokutwa bado mnataka kuwafunga mikono. Hofu ya nini kama unajiamini? Tuingie 'field' (eneo la kazi) tunaone shughuli inavyokuwa pevu," alisema Mbowe.

Aidha, aliwataka viongozi kutambua kuwa uchaguzi huo si lelemama na kwamba Chadema inajiandaa pasipo kupigana na mtu bali kutafuta haki.

"Vikao vya kupeleka rufani ni utaratibu lakini kuna maelekezo maalum yametolewa ya kuwaengua wagombea wetu. Kumwona kamanda wa polisi amekuja kwenye kikao cha ndani cha chama unafikiri ni bahati mbaya? Eti anatupenda sana?" Alihoji huku wanachama wakicheka na kumkaribisha kwa kusema: “Mgeni wetu karibu sana”.

"Kuna vihunzi vingi tulivijua mapema kama vya kadi, watu wakose kadi ili watu wapite bila kupingwa, wakijua hakuna chama cha upinzani chenye uwezo wa kutoa kadi kutoka Mtwara mpaka Kigoma mpaka Tanga. Chadema tuko vizuri,” alisema.

Mwenyekiti huyo baada ya kuzungumza hayo, alisema ameyazungumza hayo kama tahadhari ili wanachama na viongozi wa Chadema wajipange mapema, ili wagombea wa chama hicho wasije wakaenguliwa pasipo sababu za msingi.

Jana, mkutano huo uliendeshwa kwa saa kadhaa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Jeshi la Polisi wakiwamo askari kanzu.

Askari kanzu pamoja na askari waliokuwa na silaha walivamia mkutano huo saa 5:00 asubuhi na kuingia ndani ya ukumbi na kuhojiana na baadhi ya viongozi na baadaye kuimarisha ulinzi kila kona ya eneo hilo hadi saa 10 jioni.

Wakati Polisi wanazingira ofisi za Chadema zilizoko mtaa wa Gezaulole, Mbowe alikuwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu, madiwani na makatibu wa Chadema.

Polisi waliovamia mkutano huo na kuweka ulinzi mkali mwanzo hadi mwisho wa mkutano huo, walikuwa wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Hai, Lwelwe Mpina.

Nipashe ilipofika eneo hilo, ilishuhudia polisi wakiwa wameweka ulinzi zilipo ofisi hizo ambako Mbowe alikuwa ameegesha gari lake lililokuwa na utambulisho wa Kiongozi wa  Upinzani Bungeni (KUB).

Alipotafutwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, kuzungumzia hatua hiyo ya polisi alisema: "Polisi wana kazi ya kumlinda kila mtu na kuhakikisha usalama wa watu wengine. Lakini pili wanapaswa kupata taarifa ya kile kinachoendelea katika mkutano ambao ina mashaka nao, hasa kutokana na desturi yao waliyojiwekea wenyewe.

"Kwa hiyo tumepeleka polisi na wako ndani ya hiki kikao kwa kuwa ni mkutano wa chama cha siasa na si ‘send off’ (sherehe ya kumuaga binti kabla ya kuolewa) wala harusi na kama mijadala yao haina shida yoyote, basi polisi watasikia."

Alisema hata katika mkutano mingine ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), polisi wanakuwa ndani kwa hiyo hawana haja ya kuhofia kwa kuwa polisi wapo kwa ajili ya usalama.

Kwa mujibu wa Sabaya, lengo la polisi ni kuhakikisha wale watu walioko pale wako salama, lakini hawawasababishii wengine uvunjifu wa amani ndiyo maana wamewaagiza wakae pale kuhakikisha usalama wao.

Baadaye, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, akizungumzia tukio hilo, alisema haelewi ni kwa nini polisi wanavamia mkutano wao wakati ni wa ndani.

Awali, kulikuwa na taarifa kwamba katika mkutano huo, Chadema walipanga kujadili pamoja na mambo mengine, uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu.

Habari Kubwa