Wasiojulikana wachoma nguzo 60 za umeme

01Oct 2019
Said Hamdani
LINDI
Nipashe
Wasiojulikana wachoma nguzo 60 za umeme

SERIKALI imeendelea kukemea vitendo vya uharibifu wa mazingira, ukiwamo uchomaji moto misitu unaofanywa na baadhi ya jamii kwa kuwa wamekuwa wakisababisha kuharibu miundombinu inayotekelezwa na serikali.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya wawekezaji, serikali na wafanyabiashara, uliofanyika Manispaa ya Lindi.

Mgalu alionyesha masikitiko hayo kufuatia watu wasiofahamika kuunguza nguzo 60 za umeme eneo la Kata na Tarafa ya Pandeilaya, Kilwa mkoani Lindi.

Hata hivyo, Mgalu hakubainisha hasara iliyopatikana kufuatia uharibifu huo.

Mgalu alisema: “Hivi sasa nipo hapa mkutanoni napokea ujumbe kwamba kuna nguzo 60 za umeme zimechomwa moto huko Pande.”

Mgalu amesema kutokana na uharibifu huo, zinahitajika zaidi ya Sh. milioni 30 kuirejesha hali hiyo, na kuwa hali hiyo  inarudisha nyuma jitihada za serikali katika kuwaondolea wananchi changamoto zinazowakabili za kukosa huduma ya umeme.

Pia aliwaomba viongozi wa Mkoa wa Lindi, wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya upelelezi kwa lengo la kuwabaini wahusika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Lindi, Felician Makotta, alipoombwa kutoa ufafanuzi juu ya tukio hilo, alisema nguzo zilizoungua bado zipo chini ya mkandarasi anayemiliki Kampuni ya State Grid iliyopewa kazi ya kusambaza umeme maeneo ya vijijini.

“Ni kweli taarifa aliyoitoa Naibu Waziri wetu, lakini bado nguzo hizo zipo chini ya mkandarasi aliyepewa kazi ya kusambaza huduma hiyo maeneo ya vijijini,” alisema Makotta.

Mwandishi wa Habari hizi alipowasiliana na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Charles Mlawa, alikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini hakutaka kutoa maelezo zaidi, badala yake alimtaka kuwasiliana na meneja wake, Bahati Manyangali aliyeko eneo la mradi.

Hata hivyo, Bahati alipotafutwa kupitia simu ya mkononi, sinu iliita muda mrefu bila kupokelewa.

Habari Kubwa