Mabilioni uhujumu uchumi kufanya makubwa

01Oct 2019
Romana Mallya
Nipashe
Mabilioni uhujumu uchumi kufanya makubwa

KIASI cha Sh. bilioni 107.8 kilichotangazwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, kinachotarajiwa kurudishwa na watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi, kitawezesha serikali kujenga vituo vya afya 215 na hospitali 56 za wilaya.

Rais John Magufuli na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga.

Kwa mujibu wa Mganga kiasi hicho kingetokana na watuhumiwa wa uhujumu uchumi 467 ambao wamejitokeza kuandika barua za kuomba msamaha.

Tathmini iliyofanywa na Nipashe imebaini kuwa kama kiasi hicho kingepatikana kingeleta mabadiliko makubwa katika sekta za afya na miundombinu.

Jana, Rais John Magufuli akizungumza baada ya kupokea taarifa ya DPP, alisema fedha zinaweza kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kama afya, barabara na kulipa mishahara ya watumishi.

Nipashe imebaini kuwa makadirio ya ujenzi wa kituo kimoja cha afya ni sawa na Sh. milioni 500 ambazo zikigawanywa zinaweza kujenga vituo vya afya 215 na kila kata kupata kituo kimoja.

Pia kiasi hicho cha fedha kikiingizwa kwenye ujenzi wa hospitali za wilaya, kitawezesha wilaya 56 kuwa na hospitali.

Kadhalika, Nipashe imebaini kuwa iwapo fedha hizo zitaelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami, zitawezesha kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 103 (kwa mfano, kutoka Dar es Salaam – Chalinze).  Kilomita moja ya barabara ya kiwango cha lami inagharimu Sh. bilioni moja.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alimpongeza DPP pamoja na watendaji wake kwa kazi wanayoifanya na kwamba idadi hiyo ya watuhumiwa 467 iliyojitokeza kuitikia ushauri alioutoa, hakuitegemea.

"Sikutegemea kama watu wengi wangejikotekeza, watuhumiwa 467 wa kesi za uhujumu uchumi wameandika barua wakiomba wasamehewe na kulipa fedha wanazodaiwa kwa awamu, kadiri watakavyokuwa wamekubaliana nyinyi na serikali, kwa kweli sikutegemea.

"Jumla Sh. 107,842,112,744.4 zitapatikana, nikupongeze DPP pamoja na watendaji wenzako wanaokusaidia kwenye ofisi yako, ninawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya nasema kwa dhati ofisi yako inafanya kazi kubwa," alisema na kuongeza:

"Kwanza nikiri sikutegemea kama wangejitokeza watu 467 mpaka sasa na umeeleza wengine wameshindwa kwa sababu mchakato wa kuandika barua kwenye magereza wengine wamecheleweshwa na kuna barua ambazo hazijafika, ambazo zimekwama magerezani.

"Kwa hiyo kuna barua za watu wanaoomba msamaha zimekwama kwenye ofisi zako za mkoa na nyingine zimekwama magerezani, na umechomekea hapa nikuongezee siku tatu.”

"Kwanza, huu mwitikio ni mkubwa sana wa watu 467 na kama kweli wapo waliokwamishwa na wamekwama kutokana na umbali kutoka mikoani kuja hapa na wengine kwenye mchakato ndani ya magereza na umeniomba siku tatu, hakuna tatizo, mimi naomba nikupe siku saba, ili usiniombe siku nyingine."

Rais Magufuli alisema alitoa siku siba za awali ili watuhumiwa wote wanaotaka kupata msamaha kwa kupitia mchakato wa kisheria, wafanye hivyo na wameitikia na fedha Sh. bilioni 107.8 zitaokolewa.

"Nina uhakika hawatarudia makosa yao, ninafikiri niwaongezee siku saba zaidi, lakini nitoe tahadhari, baada ya siku hizi kuisha wale wote watakaohusika kwenye masuala ya uhujumu uchumi, sheria ichukue mkondo wake.

"Isije ikawa imejengeka mazoea, kwamba kesi ya uhujumu uchumi haipo, watakaoshikwa baada ya siku hizi saba nilizoongeza na wale ambao wana kesi mpya, kwa sababu leo mtu akihujumu apelekwe kwenye kesi hausiki na huu msamaha."

SIKU SABA BASI

Alisisitiza kuwa katika kesi za uhujumu uchumi watu watakaoshikwa kuanzia jana na kuendelea waendelee nazo.

"Siku saba ambazo nimeongeza kwa wale ambao wamekwama, wameandika barua lakini bado zipo magerezani hazijakufikia (DPP), lakini zimeandikwa na wale ambao wameandika lakini barua zipo kwenye ofisi zako za mikoani.

"Inawezekana mwingine akawa amejifikiria zaidi katika siku ya leo (jana) hadi siku ya saba akatoa maamuzi yake."

WANAODANGANYWA

Rais Magufuli alisema anafahamu wapo wanaodanganywa, wanaambiwa msamaha ni wa uongo.

"Hakuna msamaha wa uongo, ukishatoa msamaha ni msamaha, huwezi ukatoa msamaha wa majaribio, huwezi ukatoa msamaha wa kumtega mtu, msamaha ukishatoa ni msamaha, kinyume na hapo labda wewe unayeutoa utabeba hiyo dhambi kwa Mungu," alisema.

Alisema anafahamu wapo wengine wanadanganywa na mawakili wao ili waendelee kuwachomoa fedha watu hao.

"Wanawaambia ukiomba msamaha maana yake umejishtaki mwenyewe, hao shauri yao wachague kusikiliza mawakili wao au wachague kukusikiliza DPP na ushauri wangu nilioutoa, ndio maana ninasema nimetoa siku saba nyingine, sitatoa tena," alisisitiza.

Kuhusu waliojitokeza kuomba msamaha, Rais Magufuli aliwapongeza kwa kuandika barua na kuiomba ofisi ya DPP iharakishe ili watu waanze kuwa huru, watoke wakajumuike na familia zao.

"Mtu akishalipa fedha na mkishafanya michakato yote ya kimahakama, kwa sababu waliingia kwa njia ya mahakama watatoka kwa njia ya mahakama, muwahishe haraka kwenye vyombo vya sheria ili waachiwe, wakajumuike na familia zao, isije hawa 467 mtakapochambua labda mkajikuta wamebaki 400 au 300 wakakaa tena wanasubiri, ilikuwa wiki, ikawa wiki mbili, mwishoe mwezi, hadi mwaka, dhana ya msamaha haitakuwa na maana," alisema.

Alimweleza DPP kuwa anaamini ofisi yake imejipanga vizuri na hatua itakuwa ni kutoa msamaha.

"Wapo walioshikiliwa na maofisa wa magereza kwamba sipeleki ombi lako lazima na sisi unatuachaje tunaokushikilia…, Kamishna wa Magereza upo hapa? Fuatiliane wote waliopo magereza ambao wameomba msamaha huu kwa DPP ili msiwakwamishe,” alisisitiza.

"Ili watu kwa dhamira yao wala msiwalazimishe, pasitokee mtu wa kulazimishwa kuomba msamaha kwa hiari yao katika siku hizi, nafikiri ni kitu kizuri hizi Sh. bilioni 107 zitatumika kujenga hospitali, barabara na kulipa mishahara ya wafanyakazi.

Alisema watuhumiwa hao, walikuwa na shughuli na biashara zao zilikuwa zimekwama, waje washiriki pamoja na serikali katika kuziendeleza na serikali ikusanye kodi.

"Lengo letu kubwa ni kujenga nchi yetu, nilifikiri DPP mkashirikiane na ofisi nyingine, kama kesi ilikuwa ikisimamiwa na ofisi ya Takukuru mkashirikiane vizuri kwa vile DPP amesharidhia kwamba anataka kuwasamehe kwa mujibu wa sheria na taratibu basi mkashirikiane nao, kama ni suala la upelelezi Jeshi la Polisi au Magereza mkashirikiane," alisema.

AWAONDOA WASIWASI

Aliwahakikishia wanaotubu makosa yao na kurudisha walichokiri wasiwe na wasiwasi.

Alisema hawezi kufanya kazi ya kitoto, siyo kwa wakati huo na kwamba akishasema ametoa msamaha maana yake ni msamaha kweli.

"Msidanganywe, hao wanaowadanganya wanataka mwendelee kukaa gerezani, na kadiri mtakavyokaa msimlaumu mtu yeyote, DPP amesharidhia ameguswa na Watanzania wengi wangependa kuwaona hao watu wakirudisha na kutubu dhambi zao, lakini hatuwalazimishi.”

"Nitoe angalizo kwa DPP kwa wale wanaoshikwa na kesi za uhujumu uchumi, wasifikiri wanahusika na msamaha huu, kashughulike nao kisawasawa, siyo kwamba kesi za uhujumu uchumi zimefutwa.”

"Ziliundwa kwa mujibu wa sheria, ila kwenye hili nilitoa ombi na ombi limekubalika kwako na wasaidizi wako, na mtu mwenye mamlaka ya kufuta kesi yoyote ni DPP wala siyo mtu yeyote, pamoja na mahakama inayotoa hukumu."

DPP AMWAGIWA SIFA

Rais Magufuli alisema wamekuwa wakishuhudia na kusikia jinsi ofisi hiyo ikifanya kazi vizuri hasa katika kesi na mashauri mbalimbali na mara nyingi serikali imekuwa ikishinda kwa sababu ya uwakilishi mzuri kwa niaba ya Watanzania.

"Tumeshuhudia madini yakitaifishwa, na hii inadhihirisha ni namna gani ofisi yako inafanya kazi kubwa katika kutetea serikali na rasilimali za Watanzania.”

"Ninawaomba mwendelee hivyo, ninawapongeza PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambao nao wamekuwa wakishiriki kwenye kesi, Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha upelelezi, endeleeni kushikamana kwa pamoja."

Pia Rais Magufuli aliwashukuru watendaji wa mahakama katika kutoa uamuzi kulingana na sheria zinazowaongoza.

Awali Mganga akiwasilisha mbele ya Rais Magufuli taarifa za watuhumiwa hao,  alimweleza kuwa katika kipindi cha siku saba alichotoa kilichoishia Jumamosi, ofisi yake imepokea barua za washtakiwa 467 wakiomba kukiri makosa yao na kurejesha fedha walizowaibia Watanzania.

"Barua hizi zimeendelea kuja, mpaka jana (juzi) bado zilikuwa zinakuja kwa sababu nyingine zimechelewa kutoka mikoani kuja ofisi yangu. Kati ya washtakiwa hao, Sh. bilioni 7.9 zinatarajiwa kurudishwa wakati wowote kuanzia sasa."

Mganga alisema kwa washtakiwa wengine fedha zinazotarajiwa kurudishwa ni Sh. bilioni 5.7.

"Katika kundi hilo, wako ambao tayari wanataka kurudisha moja kwa moja bila kulipa kwa awamu, ambazo ni Sh. bilioni 13.6. Kundi la pili ni la watu ambao wanataka kulipa kwa awamu jumla yake ni Sh. bilioni 94.2.

"Ukijumlisha washtakiwa wote 467, jumla ya fedha ambazo washtakiwa wapo tayari kurudisha ni Sh. 107.8."

Alisema Ijumaa iliyopita mtu aliyekuwa akidaiwa Dola za Marekani 450,000 aliitikia wito huo wa Rais Magufuli na kuamua kukiri kosa lake mahakamani na kuzilipa fedha hizo moja kwa moja kwa aliyekuwa akimdai na faini ya Sh. bilioni tano.

"Ijumaa hiyo hiyo kuna mtu alikuwa na gramu 2123.64 za madini vito vyenye thamani Dola za Marekani 15876.66 ambaye naye alikiri makosa na kulipa fedha hizo na madini hayo kutaifishwa.

"Katika zoezi hili kati ya wanaokubali kulipa na kurejesha mali kuna gramu 33.2 za dhahabu na kilo 18 za madini aina ya Tanzanite zilizokamatwa Arusha na tukijumlisha na kilo 35 za madini vito, watuhumiwa wapo tayari kuzirudisha."

"Tunalazimika kuyasoma majalada, kuyachambua vizuri na kuyapitia kwa kina ili kuona ni maeneo yapi ambayo tunaweza kukubaliana nayo na yapi hatukubaliani nayo na kurekebisha aina ya mashtaka na kwenda nayo mahakamani kwa mujibu wa sheria ili  kesho na kesho kutwa wasije wakatumia mbinu nyingine kuishtaki serikali," alisema.

Alimweleza Rais Magufuli kuwa changamoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na kupitia barua ambazo nyingine zimeandikwa kwa mkono.

"Nchi yetu ni kubwa kiasi kwamba wengine walioko gerezani walikuwa wanakosa nafasi ya kuandika mapema kwa sababu katika siku hizo kuna wengine walikuwa wanahudhuria kesi mahakamani na hawakupata nafasi ya kuandika barua.”

"Kama utaridhia, Mheshimiwa Rais, ninaleta ombi kwako kwamba utuongezee siku tatu na wakati huo huo na sisi tunaendelea kukamilisha kazi tuliyokuwa nayo ili kuhakikisha hayo majalada tunayasoma, tuanze kwenda mahakamani hatua kwa hatua," alisema.

Habari Kubwa