Waziri Mkuu kufanya ziara siku nne Singida

01Oct 2019
Elisante John
SINGIDA
Nipashe
Waziri Mkuu kufanya ziara siku nne Singida

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufanya ziara ya siku nne ya kikazi katika Mkoa wa Singida, kwa ajili ya kukagua na kutembelea miradi ya maendeleo, ikiwamo mikubwa ya kitaifa,  pamoja na kufungua maonyesho ya SIDO kitaifa mjini Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alisema jana kuwa ziara ya Majaliwa itaanza Ijumaa katika Wilaya ya Manyoni, akitokea mkoani Dodoma na kuhitimisha Oktoba saba.

Alisema siku ya kwanza Waziri Mkuu atatembelea pia Halmashauri ya Itigi, Oktoba tano atafanya ziara kwenye Halmashauri za Wilaya ya Ikungi na Manispaa ya Singida, na kuwa Jumapili  ataendelea na ziara wilaya za Mkalama na Iramba.

Dk. Nchimbi alisema Waziri Mkuu atahitimisha ziara hiyo Jumatatu kwa kufungua maonyesho yaliyoandaliwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) katika viwanja vya Bombadia mjini Singida, yatakayomalizika Oktoba 9.

“Katika ziara hii, Waziri Mkuu atakagua na kutembelea miradi ya kimkoa, kukagua na kuona nini kinachofanyika kwenye miradi ya kitaifa, ukiwamo ule wa umeme wa kilovolti 400 unaopokea na kupoza umeme, ambao utasambazwa kwenda hadi nchi jirani kwa ajili ya kuuza,” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa alifafanua kuwa pia kwenye ziara hiyo Waziri Mkuu atakagua daraja la mto Sibiti linalounganisha mikoa ya Singida na Simiyu, ambalo limeshakamilika, huku likiunganisha barabara inayokwenda nchi jirani.

Alifafanua kuwa, kazi kubwa iliyobakia ni kuweka lami kipande cha barabara kilomita 20 za maingilio kwenye daraja hilo, hivyo kuzidi kuchochea uchumi wa wananchi wa mikoa hiyo na taifa kwa ujumla.

Aidha, Dk. Nchimbi alisema kwenye ziara hiyo, Majaliwa atatembelea kiwanda cha kampuni ya Biosssitine kinachochambua pamba katika Manispaa ya Singida, ambacho pia kinanunua na kutengeneza mbegu za zao hilo na kusambazwa kwa wakulima nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Prof. Sylvester Mpanduji, alisema maonyesho ya mwaka huu yatakuwa na mvuto mkubwa, kutokana na ushiriki wa mataifa makubwa ikiwamo China, India na Afrika Kusini, ambazo zimepiga hatua kubwa, kwa teknolojia ya viwanda.

Habari Kubwa