Tuwaepushe wazee na tiba za waganga 

02Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tuwaepushe wazee na tiba za waganga 

KUZUIA maradhi na kuhakikisha wazee wanakuwa na afya bora ni suala ambalo linastahili kuwa la kipaumbele wakati huu serikali na jamii inapoadhimisha Siku ya Wazee Duniani.

Ndiyo maana tunaweza kusema  uzee bila tiba ni kama  uzee uliodharauliwa kwa sababu unapokuwa na umri huo ndipo milango ya maradhi na kudhoofika kiafya inapofunguka.

Taifa lipowakumbuka wazee leo, hebu tutizame hali zao na jinsi walivyo na mchango mkubwa kwa taifa letu.

Itakumbukwa kuwa wazee hawa wanashambuliwa na magonjwa na wengi huendelea kujitibu kwa mitidawa na huduma nyingine za tibaasilia.

Ni ukweli usiopingika kuwa wazee wa taifa hili wanahitaji huduma na utaratibu ambao utafanya maisha yao kuwa myepesi hasa kwenye kupata tiba.

Ndiyo maana tunaona kuwa tunapoadhimisha siku ya wazee wetu , tutafakari jinsi ya kuwaondoa kwenye giza la tiba za asilia na hata wakati mwingine kukimbilia kwa waganga wa ramli.

Wazee hawa wake kwa waume, mara nyingi tunawashuhudia, ambavyo  wamekuwa wakisota iwe kwenye zahanati, hospitali za wilaya, mikoa na hata za rufani  bila kupata huduma licha ya kuwa na kadi za wazee.

Mara kwa mara wale ambao watoto wao au jamaa zao hawakuwaingiza kwenye mfumo rasmi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), tumewashuhudia wakihangaika mno kusaka tiba.

Wazee hao ambao mara nyingi inakuwa vigumu kupata vipimo vikubwa hata pale wanapotumia kadi za Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii Ulioboreshwa, wanahitaji kufikiriwa upya sasa kuhusu matibabu.

Ndiyo maana tunaona kuwa pengine ni wakati wa kufikiria namna bora ya kuwa na Mfuko wa Bima ya Afya Wazee kama ambavyo kuna toto afya kadi ya watoto wadogo na walio chini ya miaka 18.

Tunasema hivyo kwa sababu ni vigumu wazee hawa waliolitumikia taifa kwa miongo kadhaa kuwa na uwezo wa kujigharamia matibabu kwa jinsi ya hali halisi ilivyo sasa.

Licha ya  huduma ya toto afya kuondoa baadhi ya tiba muhimu kama Xray ya MRI, kipimo cha CT Scan, kusafisha damu, tiba ya saratani , tiba ya moyo, kutibu na kupandikizwa figo tunaona kwa wazee ndiyo mambo wanayoyahitaji.

Ni kwa sababu wazee hawa wanahitaji kufanyiwa vipimo kama vya MRI, CT Scan na hata kupewa dawa za saratani kwa kuwa maradhi hayo huambatana pia na umri wa uzee.

Ni vyema serikali ikakubaliana nasi kuwa iwapo taifa litaamua kuwa na kadi ya matatibabu ya wazee ni muhimu ikaandaaliwa kwa kutumia mfuko wa NHIF kama ilivyo ya watoto.

Ni muhimu kuangalia upya matibabu ya wazee hawa  kwa sababu kama tulivyotangulia kusema tiba ni suala linalowaumiza wazee wengi mno hapa nchini.

Ni ukweli kuwa hata kama utafiti ungefanyika leo wazee wengi wangebainika kuwa na udhaifu kutokana na kudhoofishwa na magonjwa.

Licha ya kwamba chakula na umaskini ni suala linalowakabili wazee wa Tanzania, tiba ni jambo muhimu kwa ajili ya ustawi wa kundi hili.

Ndiyo maana umefika wakati wa kuanza utaratibu wa kuwatibu pengine hata kwa awamu. Serikali kuanzia sasa ianze mikakati ya kuandaa mfuko wa bima ya wazee kwa ajili ya ustawi wao.

Kuna mambo mengi yanayofanyika na yanagharamiwa na serikali ikiwamo mfuko wa barabara, mfuko wa mahakama na maeneo mengine kama hayo, hivyo ni wakati wa kuwakumbuka na kuwasaidia wazee.

Shime serikali iwakumbuke wazee hawa na kuwaondolea mzigo wa kikimbilia kwa waganga wa kienyeji na kula tiba za asilia ambazo mara nyingi haziwaponyeshi.

Habari Kubwa