TCRA mkoa wapi wakati tunaibiwa?

02Oct 2019
Salome Kitomari
Nipashe
TCRA mkoa wapi wakati tunaibiwa?

KATIKA kikao cha Bunge la Bajeti, Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe, aliwasilisha kilio chake dhidi ya kampuni za simu kuwaibia wateja wake vifurushi na muda wa maongezi, na alijibiwa kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Mbunge huyo ambaye amewahi kuwa Waziri katika serikali ya awamu ya nne na tano, alisema kampuni hizo pia zinadanganya watu kwa kununua vifurushi.

Si ajabu pale mtu kwa mfano ana dakika 200, lakini anapokuwa ametumia dakika 45 kwa kufuatilia anaambiwa kuwa dakika zake zimekaribia kwisha!

Kilio cha Mbunge huyo ndiyo kilio cha watumiaji wengi wa simu nchini kwa kuwa kila siku wanayavumilia mengi yanayotendwa na kampuni za simu dhidi yao.

Mathalani, ipo kampuni moja ya simu wasione una salio kwenye mtandao ni lazima wakuonyeshe kuwa umeishiwa kifurushi na muda wa maongezi.

Ukiwauliza jibu lao siku zote ni rahisi sana kwamba muda wa maongezi au bando kwisha hutegemea na matumizi yako, hivyo unapoona imekuwa hivyo ujue matumizi yako ni makubwa.

Unaponunua muda wa maongezi kutoka kwa kampuni hizo unaokwenda sambamba na bando, ikitokea bando limekwisha basi muda wa maongezi nao umekwisha, na wakati mwingine bando likiisha na muda wa maongezi nao umekwisha.

Aidha, kampuni hizi zimeanzisha utaratibu wa kumwezesha mteja kununua muda wa maongezi moja kwa moja kutoka kwenye salio lake la simu, lakini kuna nyakati hawezi kufanya hivyo kwa kuwa wanataka ahamishe fedha hiyo kwenda kuwa muda wa maongezi ili akatwe kodi kwanza.

Mathalani, unanunua muda wa maongezi wa Sh. 5,000 kodi yake ni Sh 762.71 maana yake unapaswa kununua zaidi ili kufidia gharama hizo zinazobwebwa na mtumiaji wa simu na kuwa maumivu kwake.

Wakati mwingine unapokuwa na salio kwenye simu yako ni lazima uzime data, ukinunua salio huku data inafanya kazi unajikuta salio lote limeisha ndani ya sekunde chache, na ni kawaida kuchukua saa kadhaa kujiunga kupata vifurushi.

Kama haitoshi kuna wakati mtandao unagoma kubadilisha kifurushi, unaweza kununua zaidi ya mara nne na hupati ujumbe wa kubadilisha kwenda kwenye kifurushi na ukijaribu kupiga simu, unachukuliwa fedha yote iliyomo kwenye simu yako.

Unapojaribu kuwapigia huduma kwa wateja hupati majibu ya kuridhisha, na matokeo yake watumiaji wa simu wanaendelea kuumia kila siku.

Miezi miwili iliyopita, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasililiano, alizionya kampuni za simu zilizokuwa zinatoza zaidi ya bei elekezi ya Sh 10.40.

Aidha, kuna kampuni zinazojinadi gharama ya mtandao wowote ni Sh. moja kwa sekunde ambayo ni sawa na Sh. 60 bei ambayo inazidi mara tano ya gharama ambayo ni elekezi.

Alisema bei elekezi imepungua kutoka Sh.15.60 hadi Sh. 10.40, huku malengo ya serikali ni kuwa ifikapo 2021 kampuni zitoze Sh. 2 kwa dakika kwa mtandao wowote wa simu.

Aliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuchukua hatua dhidi ya wahusika na kuhakikisha wateja wanarudishiwa fedha zao walizoibiwa kwa muda mrefu.

Licha ya serikali kutoa onyo na Bunge kulalamikia suala hilo na kuelekeza hatua kuchukuliwa, lakini bado wateja wanaendelea kuumia na kukosa pa kupeleka kilio chao.

Kwa ujumla watumiaji wa simu kila mmoja kwa nyakati zake ana kilio dhidi ya kampuni hizo, lakini cha kushangaza hatuoni hatua zinazochukuliwa au ahueni kwa watumiaji wa simu.

Wizi wa bando na dakika ni tatizo kubwa kwa mitandao ya sasa kiasi cha kujiona wanyonge, na wakati mwingine hakuna la kufanya kwa kuwa ni lazima mtu awasiliane kupitia simu.

Muungwana anaona kwamba ni vyema basi kwa msimamizi wa kampuni hizo ambaye ni TCRA akachukua hatua dhidi ya kampuni hizi, kuliko watu kuendelea kuumia kimya kimya.

Habari Kubwa