Wahudumu wa afya nchini mmemsikia Waziri Mkuu?

03Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Wahudumu wa afya nchini mmemsikia Waziri Mkuu?

MSIMAMO wa serikali inavitaka vituo vyote vya umma kutoa huduma bora na za haraka kwa wazee wenye vitambulisho, pia vitenge dirisha maalumu kwa ajili yao.

Lengo la kufanya hivyo ni kuwafanya wazee wasiwe na muda mrefu kwenye foleni wanaposubiri kupata huduma hizo za afya, hali inayoweza kuwasababishia usumbufu usio wa lazima.

Mbali na hilo, halmashauri zote nchini zinaagizwa kuhakikisha zinafanikisha utambuaji na kuwapatia vitambulisho wazee wasio na uwezo, linakuwa endelevu kwa ajili ya kuwanufaisha bila ya malipo, pindi wanapougua.

Kupitia maagizo hayo, ni wazi baadhi ya watendaji wa serikali wenye dhamana za kuamua, kama vile wakurugenzi wa wilaya wamewahi kulalamikiwa kukwamisha Sera  Taifa ya Wazee ya Mwaka 2007, watakuwa wamemwelewa.

Hiyo ni kauli ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa mkoani Mtwara katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani, ambako ndiko kulikufanyika hafla ya kitaifa.

Kiongozi huyo, anawaambia Watanzania kwamba serikali itaendelea kuwalinda wazee dhidi ya vitendo vya ukatili, kwa kuwawekea miundombinu na mazingira bora yanayolinda nafsi zao.

Mazingira bora yanatajwa ni katika mazingira kama vile matumizi ya vyombo vya usafiri, pia kuwekwa utaratibu na vigezo vya kuwawezesha kulipwa pensheni, pia mashirika ya wazee yaelekeze rasilimali wanazozipata kutoa huduma za msingi kwa wazee.

Njia mojawapo ya kufanikisha anayoitaja Waziri Mkuu, ni kuepuka kutumia fedha nyingi kwenye mikutano, warsha na kongamano, yasiyowafaidisha moja kwa moja wazee wenye uhitaji maalum.

Anaeleza kuwa utoaji huduma kwa wazee, ni moja ya vipaumbele vya serikali na kwamba itaendelea kuchukua hatua kuboresha maisha yao, ikiwamo kuimarisha ustawi na maendeleo yao.

Nikirudia hoja husika, ni kwamba hatua zinazochukuliwa na serikali kwa sasa ni wazi malalamiko yao ya muda mrefu yanaweza kupungua, kama siyo kumalizika kabisa.

Kinachotakiwa kufanywa ni wahusika kuzingatia maelekezo ya serikali, ili kuwaondolea wazee usumbufu ambao wamekuwa wakiupata wanapokwenda kwenye vituo vya afya kupata matibabu.

Changamoto ambayo wazee wamekuwa wakikutana nayo kwenye baadhi ya vituo vya afya, ni kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu kusubiri huduma na wakati mwingine wanakosa hata sehemu ya kukaa.

Hali hiyo, inawalazimu wakati mwingine wasimame kwa muda mrefu kwenye foleni wakisubiri kumuona daktari, lakini kama wangepewa kipaumbele, vituo vya afya visingelalamikiwa kama inavyosikika kila siku.

Jambo la kuzingatia ni kila mtu kwa nafasi yake akumbuke kuwa ipo siku atakuwa mzee, panapo majaliwa ya Mwenyezi Mungu kama atafikia umri huo.

Pia watoa huduma za afya watambue miaka itakwenda, nao watazeeka na wajibu wao pia unawataka kuwahudumia wazee hao na katika mazingira hayo, watahitaji kuhudumiwa au kupata huduma za afya bure.

Niseme, kwa mustakabali huo, hao wahumdumu wa afya, kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakielekezwa kwao.

Ikumbukwe, serikali ilishatoa maelekezo kupitia mwongozo wa matibabu bure kwa wazee wenye umri kuanzia miaka 60, wanatakiwa kupata huduma za afya bure katika hospitali zote za umma.

Hata hivyo, utekelezaji kwenye baadhi ya maeneo umekuwa ukilalamikiwa kuwa bado ni wa kiwango cha chini, huku ikidaiwa wazee wanalazimika kutoa fedha kununua dawa.

Bado ninaamini hatua ya serikali kutaka vituo vya afya kutoa huduma bora na za haraka kwa wazee katika dirisha maalum, dhamira sahihi kumaliza adha hiyo.

Vilevile ni hatua nzuri ya wazee 1,837,162 kutambuliwa, kati yao 684, 383 wameshapewa vitambulisho kuwawezesha kupata huduma bila ya malipo.

Ni muhimu kuzingatia kaulimbui ya mwaka huu isemayo “Safari ya Kuzeeka Kwa Usawa” inayoonyesha kutambua malengo ya maendeleo endelevu, kwamba yatafikiwa iwapo watu wa umri wote watakuwa wamejumuishwa.

Habari Kubwa