Baada ya magogo tuangalie machinjio

03Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Baada ya magogo tuangalie machinjio

ITAKUMBUKWA kuwa  Septemba 30, 2019 ndiyo mwisho wa kutumia magogo kukata nyama kwenye mabucha.

Tunaipongeza serikali kwa kuliona hili na kuondoa utaratibu huo uliokuwa unawalisha watu  nyama zilizojaa vibanzi vya mifupa na miti, harufu au shombo kutokana na gogo kutunza nyama zilizovunda kwa muda mrefu.

Gogo hilo lilikuwa halisafishiki wala kufanyiwa usafi wa aina yoyote kwa muda wote, hata kama kulikuwa na tatizo.

Tunashukuru kwani kero haipo na sasa ni wakati wa kutumia misumeno kukata nyama, kujenga maduka yenye milango ya vioo na wavu kuzuia inzi kujaa buchani pamoja na kuwa na friji kwa ajili ya kutunza kitoweo hicho.

Tunapongeza juhudi hizo na sasa tunategemea kuona mamlaka kama Bodi ya Nyama ikifuatilia na kufunga bucha ambazo hazina viwango ili kuhakikisha afya za walaji zinazingatiwa na kila mmoja analishwa chakula bora.

Pamoja na ufuatiliaji huo tungependa kuona kuwa mashine za kukatia nyama zinapatikana na kuuzwa kwa bei isiyowaumiza wafanyabiashara, kwani inavyoelekea wengi wanatumia misumeno mikuukuu au mitumba.

Lakini, pamoja na mafanikio hayo mijini, tunaiomba serikali itizame suala hilo na jinsi ambavyo linaweza kutekelezwa vijijini kwani kutokana na ukosefu wa umeme wananchi wataendelea kulishwa nyama za magogo.

Pengine ni wakati wa Shirika la Uendelezaji Viwanda Vidogo (SIDO) na Mamlaka za Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), kuangalia namna bora ya uchinjaji nyama vijijini ambao utaepuka kutumia magogo na kuwalisha wananchi nyama zenye vimelea vya maradhi uchafu na vibanzi vya miti na mifupa.

Sido na Veta zinaweza kubuni utaratibu bora kwa ajili ya kukata kitoweo hicho ambacho mara nyingi huuzwa ‘kienyeji’ na kwa ujumla katika mazingira ambayo si salama.

Lakini, pamoja na jitihada za kuboresha mazingira ya nyama kwenye mabucha jingine ambalo ni pasua kichwa ni machinjio ambalo nalo linahitaji utatuzi kwa vile linaathiri afya za walaji.

Tunaomba kama ambavyo jitihada nyingi zinafanyika kupata maduka ya kisasa yanayotumia msumeno kukata nyama badala ya shoka, ndivyo pia kuwa na machinjio ya kisasa yanayofuata taratibu zote za kitaalamu.

Mara nyingi tumesikia kuhusu ujenzi wa machinjio ya kisasa kama mpango uliotangazwa wa kutumia ardhi ya kilichokuwa kiwanda cha nguo cha Kilitex kilichoko GongolaMboto Dar es Salaam kuweka machinjio ya kisasa.

Mara kadhaa Jiji na Manispaa zake zimetoa ahadi za kuboresha machinjio lakini hatujaziona zikileta mafanikio.

Ikumbukwe kuwa kukosekana kwa machinjio za kisasa Dar es Salaam kunasababisha wateja wa kimataifa kununua ama kuagiza nyama kutoka mataifa jirani.

Viongozi wa Bodi ya Nyama watakubaliana nasi kuwa jijini Dar es Salaam kuna maduka ya nyama ambayo kitoweo cha nguruwe huuzwa mpaka hadi Shilingi 50,000 kwa kilo.

Nyama hizo zinazozalishwa nchi jirani hutumiwa na wateja wa jumuiya ya kimataifa ambao wanajali ubora , viwango na ladha ya kitoweo ambayo hawaipati hapa Tanzania.

Tunaweza kusema kuwa hatujaona juhudi na bidii zikifanyika katika kuimarisha machinjio ya nyama  katika halmashauri zetu.

Pamoja na kwamba kumekuwa na jitihada za kuvutia wawekezaji wa kigeni kujenga machinjio ya kisasa , jukumu la kujenga machinjio ya kisasa kama kitega uchumi cha halmashauri na majiji ni jambo lisilokwepeka hata ikibidi kuingia ubia.

Tunatoa wito kwa halmashauri na mamlaka zinazosimamia kitoweo kuhakikisha kuwa sambamaba na kuboresha misumeno na kuondoa magogo, nyama nazo zinachinjwa na kuandaliwa katika machinjio safi na salama.

Habari Kubwa