Enyi wauza mkaa, elimu hii ya TFS inawahusu

04Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Enyi wauza mkaa, elimu hii ya TFS inawahusu

MATUMIZI ya nishati ya mkaa, hasa katika maeneo ya mijini yana nafasi kubwa na yamekuwa yakiongezeka na kufikia kiwango cha juu sana. Sababu kubwa ni kutokuwapo nishati mbadala yenye bei nafuu.

Kuongezeka matumizi ya nishati hiyo, kunaelezwa kuchangia ongezeko la ukataji na ufyekaji miti, pia mkaa unatengenezwa bila ya kuwapo mpango endelevu wa matumizi ya rasilimali miti, ili isiteketee.

Pia, kingine kinachotajwa kuchangia katika ongezeko la matumizi ya rasilimali miti hiyo kwenye mkaa, ni utengenezaji wake kwa njia isiyoboreshwa, hivyo kutumia miti mingi kutengeneza mkaa kidogo.

Hiyo ni kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Kusini, ambao wanasema mkaa hutengenezwa kwa matanuru, lakini kunatakiwa kuwapo utengenezaji bora wa nishati hiyo.

Ofisa Ugani na Uenezi wa TFS Kanda ya Kusini, David Namwaga, anasisitiza umuhimu wa elimu kwa wananchi, kujua jinsi ya kutengeneza matanuru bora ya mkaa.

Anasema, TFS imekuwa ikijitahidi kuwajengea uwezo wananchi kwa ajili ya uelewa wa masuala ya mkaa na kusimamia utengenezaji bora wa mkaa katika maeneo yao ili kupunguza ukataji wa miti ovyo.

"Jambo lingine ni kujenga uwezo wa kupigana na uzalishaji na utengenezaji mbovu wa mkaa pale unapotokea na kusababisha uharibifu wa ubora wa mkaa au soko la mkaa," anasema Namwaga.

Pia, anafafanua kwamba, wakala huo wa kitaifa unafanya harakati za kudhibiti uzalishaji mkaa usiozingatia taratibu, kwa ajili ya kuokoa mapato ya serikali yanayopotea kwa kutoroshwa na kutunza mazingira.

Kwa mujibu wa TFS, kuna matanuru bora ya mkaa yanayotakiwa kutumika kwa ajili ya uzalishaji bora wa mkaa, pia usajili na ukataji leseni ya biashara uzingatie taratibu na sheria ya uvunaji wa mazao ya misitu.

Tanuru linalofaa kutumika kwa hapa nchini, ni lile la asili la kichuguu-udongo lililofanyiwa maboresho ya kina, baada ya kuingizwa kwa vipengele vikuu viwili vya tanuru la aina ya ‘CASAMANCE’ au Tanuru la Senegal.

Namwaga anaeleza kwa kutaja vifaa vinavyohitajika, ili kutengeneza tanuru lililoboreshwa kuwa jembe kwa ajili ya kusafishia eneo na kuchimba udongo, chepe la kuchota udongo wa kulifunika.

Kingine kinachohitajika katika tanuru hilo, kinatajwa kuwa ni ‘futi kamba’ ya kupima ukubwa wa tanuru, bati la futi 6.8 au 10 ili kutengenezea pa kutoa moshi, tupa, nyundo, tindo, viatu-bati na kofia.

Mjadala huu unaunga mkono juhudi za TFS kulinda misitu hasa wakati huu ambao bado hakuna nishati mbadala wa uhakika, ingawa ukataji miti kwa ajili ya mkaa umekuwa ukipigiwa kelele kwamba unaharibu mazingira.

Biashara ya mkaa ina soko kubwa. Katika wakati huu ambao hakuna nishati mbadala, ni vyema wafanyabiashara wakazingatia uvunaji na hata uchomaji, ili kutokata miti mingi kama TFS inavyoelekeza.

Katika kukabiliana na uharibifu wa mazao ya misitu, serikali ilitangaza kanuni mpya kwa ajili ya kuongeza usimamizi wa sheria kwa wanunuzi na wauzaji mazao hayo, ikiwamo mkaa na samani mbalimbali.

Hiyo ni tangu mwezi Mei mwaka huu, ilipotangaza kupitia tangazo la serikali, adhabu kwa atakayekuka kanuni hizo ni faini ya Sh. 500,000 hadi Sh. milioni 12 au kifungo kati ya miezi sita hadi miaka mitano.

Juhudi hizo zote ni kwa ajili ya kuokoa misitu na hata kama inakatwa, basi iwe ni kwa kufuata utaratibu uliowekwa, ili kulinda mazingira, badala ya kuyaharibu kama ambavyo inatokea kwenye baadhi ya maeneo.

Kimsingi, elimu inayotolewa na TFS kama itazingatiwa kuanzia kwenye uvunaji misitu hadi kuchoma mkaa, kutakuwapo uhakika mkubwa katika utunzaji misitu nchini.

Huko nyuma, taarifa iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, jijini Dar es Salaam, ni kwamba mkoa Dar es Salaam unaongoza kwa matumizi ya nishati ya mkaa, ikimaliza tani 500,000 kwa mwaka.

Hivyo, wakati mkaa ukiendelea kuwa na nafasi kubwa katika matumizi ya kila siku, ni vyema kuzingatia hatua zinazosaidia kupunguza changamoto za uharibifu wa mazingira na ukataji ovyo wa miti.

Habari Kubwa