Kama viroba viliondoka mataputapu ni ya  nini?

04Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kama viroba viliondoka mataputapu ni ya  nini?

KATIKA moja ya taarifa zetu za jana kulikuwa na habari ya kuiomba serikali kudhibiti utengenezaji wa pombe za kienyeji ambazo kwa hakika ni chanzo cha matatizo ya kiafya.

Pombe kama gongo, mbege, ulanzi, boha na chimpumu zimekuwa zikizalishwa Dar es Salaam na kwenye miji mingine mikubwa licha ya kwamba ziko kwa wingi vijijini na ndiyo maeneo yenye wanywaji wengi.

 

Aidha, kwa kuona kilio hicho nasi tunaungana na wadau hao wanaojali afya za walaji kuiomba  serikali kupinga matumizi ya vinywaji hivyo ambavyo si kwamba tu ni hatari kwa binadamu bali pia ni mwanzo wa udhalilishaji watoto na wanawake vilabuni.

 

Tuanze na suala la afya, pombe hizo hutengenezwa katika mazingira duni, hutumia maji machafu na uandaaji wake wakati mwingine hufanyika porini na vyombo vinavyotumiwa ni vichafu na wapo wanaotumia au kuchanganya pombe hizo na sumu.

 

Suala la sumu lilijitokeza miaka ya karibuni wakati watu zaidi ya 15 walipofariki Kimara jijini Dar es Salaam baada ya kunywa gongo iliyochanganywa na sarafu za senti tano,  dawa ya madoa ya jiki na pia iliwekwa kwenye matangi ambayo huenda yalikuwa na sumu ya sulphonic acid’  ambayo hayakusafishwa kikamilifu.

 

Kuna wanaosema kuwa hata taka za chooni hutumiwa kupika gongo, pumba  na taka nyingine au hata unga wa kiwango duni uliovunda nao hutumiwa kupika komoni ambayo hadi kuchachuka hupitia hatua mbalimbali kama vile kuvunda na kuwa na wadudu kama sumu kuvu.

Wasimamizi wa afya watakubaliana nasi kuwa pombe hizo huandaliwa kwenye mazingira ya ajabu ikiwa ni pamoja na ulezi au mtama kuanika na vimea vyake kutandazwa kwenye mikeka kwenye mazingira machafu.

 

Mikeka yenye vimelea hivyo huwekwa pembeni ya barabara na kwenye viwanja  au maeneo ya wazi ambayo huchafuliwa na vumbi, vinyesi vya wanyama na ndege na wakati mwingine vumbi la injini za magari.

 

Maji yanayotumiwa kuzichuja ni machafu ya mtoni au mabwawani na hata uchujaji wake ni wa kiwango duni unaotumia mashuka au viroba.

 

Aidha, uuzaji wa pombe hizo hufanyika katika maeneo ya giza na watoto hasa mabinti hutumiwa kuuza pombe hizo zinazonywewa maeneo yasiyo na vyoo wala huduma muhimu za kijamii na wakati mwingine nyumbani kwa wafanyabiashara wanaohusika.

 

Ni sehemu ambazo mabinti wanaweza kubakwa, watoto kudhalilishwa na wakati mwingine hata kufanyiwa mambo mabaya.

 

Suala la afya ni  jambo muhimu na ni lazima kulipa kipaumbele kwani linamaliza rasilimali nyingi za taifa kutibu taifodi, kipindupindu, amiba, kuhara damu na maradhi mengi yanayotokana na ulevi kama ini na figo.

 

Tunaungana na wadau kuitaka serikali kumaliza tatizo hilo kwani kama pombe za viroba na mifuko ya nailoni lilimalizika pombe za mataputapu zinangoja nini?

 

Watu wanaokunywa mataputapu wakati mwingine hutumia vijiwe au vilabu hivyo kwa ajili ya kufanya uhalifu kama wizi na uhalifu hasa unaofanyika usiku wa manane kwa kuwa sehemu hizo mara nyingi hazina ufuatiliaji wa karibu wa vyombo vya dola.

 

Shime elimu itolewe kwa wanaoandaa pombe hizo na kukumbushwa kuwa ni mwanzo wa maradhi ili kukomesha madhara yanayotokana na pombe za kienyeji.

Habari Kubwa