Tunawatakia mafanikio wanariadha wetu, U-20

05Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tunawatakia mafanikio wanariadha wetu, U-20

KWA mara nyingine bendera ya Tanzania kupitia yosso wa Tanzania Bara inatarajiwa kupeperushwa katika fainali ya mashindano ya soka ya vijana wa umri chini ya miaka 20 (U-20) ya Afrika Mashariki na Kati itakayochezwa leo katika mji wa Jinja nchini Uganda.

Timu hiyo ya Tanzania Bara itashuka dimbani kuwakabili wapinzani wao Kenya katika fainali hizo za mashindano hayo yanayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Yosso hao wa Tanzania Bara watakutana na wenzao hao wa Kenya wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja kuanzia mechi za hatua ya makundi, lakini ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2 na majirani zao.

Inaelezwa kuwa, kikosi hicho kinachoongozwa na Mzalendo Zuberi Katwila ndio timu ambayo imelelewa kwa muda mrefu, wachezaji wake wengi wakiwa ni waliopandishwa kutoka katika kikosi cha Tanzania kilichoshiriki fainali za vijana ya umri chini ya miaka za Afrika (Afcon 2019).

Ni timu ambayo imepata uzoefu wa kucheza mashindano na mechi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.Gazeti hili tunawaombea dua na mafanikio wachezaji wa timu hiyo ili wakamilishe kazi waliyoianza na hatimaye kurejea nyumbani na kikombe cha mashindano hayo.

Kunyakua ubingwa wa mashindano hayo, si tu kutaipa sifa Tanzania, pia kutawaweka wachezaji hao sokoni kwa klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi kuwafuatilia kwa lengo la kuwasajili na hapo itakuwa ndio mwanzo wa kujipatia kipato kupitia vipaji vyao.

Huu ni wakati muhimu kwa nyota wa Tanzania kuweka historia ya kushinda kikombe hicho, na vile vile kutakiwa kujiandaa kujiunga na timu nyingine za Taifa ikiwamo ile ya U-23 na Taifa Stars.

Wanachotakiwa kukifanya yosso hao wa Tanzania Bara, ni kushuka uwanjani ikiwaheshimu wapinzani wao, kwa sababu nao wataingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kuibuka mabingwa.

Nipashe inawakumbusha yosso wa Tanzania na benchi lao la ufundi kuwa, hakuna fainali mbili, wanatakiwa kupambana kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika mchezo huo na kuwapa furaha Watanzania ambao wana kiu ya kuona timu zao za hapa nchini zinatwaa mataji mbalimbali.

Nipashe pia inapenda kuwatakia kila la kheri wanariadha watatu wa hapa nchini ambao leo usiku wanatarajiwa kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya riadha ya dunia yanayofanyika katika mji wa Doha, Qatar.

Bendera ya Tanzania katika mashindano hayo itapeperushwa na Alphonce Simbu, Augustino Sulle na Stephano Huche, ambao wote watachuana katika mbio za kilomita 42 (marathoni).

Licha ya kuwapo kwa changamoto ya hali ya joto kali ambayo ilimfanya mwanariadha wa kike, Failuna Abdi, kushindwa kumaliza mbio hizo, bado Watanzania wana imani na nyie, baada ya kufanya maandalizi mazuri kabla ya kuondoka nchini na kwenda kushiriki mbio hizo za dunia.

Hakuna jambo gumu kila mahali kwenye nia, kama iliwezekana kwa Simbu kutwaa medali kwenye mbio za Mumbai Marathon, hata leo pia wanariadha wote wa Tanzania wanaweza kufanya vizuri katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).

Tunaungana na wadau wote wa michezo nchini kuwatakia kila la kheri yosso wa U-20 pamoja na wanariadha ambao wanalitumikia taifa huko Qatar.

Habari Kubwa