Tuondokane na aibu hii

05Oct 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tuondokane na aibu hii

‘AIBU’ ni jambo la kumvunjia mtu heshima; jambo la kumtia mtu fedheha; tahayuri, soni. ‘Aibika’ ni shikwa na aibu baada ya kufanya jambo la kufedhehesha, pata aibu, fedheheka.

Mpira wa miguu, yaani kabumbu, kandanda au soka ni mchezo upendwao sana duniani. Hapa nchini, timu zenye wanachama na mashabiki wengi zaidi ni Yanga iliyoanzishwa mwaka 1936 ikifuatiwa na Simba mwaka 1935. 

Ndizo timu zilizotwaa ubingwa wa Ligi Kuu  nchini mara nyingi, Yanga ikiizidi Simba kwa kutwaa mara nyingi zaidi na sasa wakijiita ‘mabingwa wa kihistoria.’ 

Mashindano ya kimataifa, Simba ilifanya vizuri zaidi hata kufikia fainali ya Kombe la Washindi Afrika ingawa ilifungwa 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast mwaka 1993 kwenye Uwanja wa Taifa ambao sasa waitwa Uwanja wa Uhuru.

Hata hivyo Simba imekuwa ikizipa shida timu za Waarabu kwa kuzifunga ndani na nje kwenye michuano ya kimataifa. Wanapopangwa kupambana na Simba, hujizatiti sana, tofauti na wanapopangwa na Yanga.

Ingawa Yanga ilianzishwa mwaka mmoja kabla ya Simba, haijafikia hatua iliyofikia Simba kucheza fainali ya Kombe la Afrika. Ilichofanya ni kuishia robo fainali tu katika kuwania Kombe hilo maarufu la vilabu Afrika. 

Kuteleza si kuanguka. Mtu aweza kuteleza asianguke. Methali hii hutumiwa kumnasihi mtu aliyekumbwa na matatizo asikate tamaa bali aendelee. Huweza pia kutumiwa na mtu aliyekumbwa na shida kuwajuza wenzake kuwa hajakata tamaa au bado ana ujasiri wa kuendelea kupambana. 

Huenda timu zetu hushindwa kutokana na tabia ya kuamini zaidi ushirikina (tabia ya kuamini uwezo wa kiumbe kingine/chengine juu yako badala ya ule wa Mwenyezi Mungu)! Kadhia (tukio la kuhuzunisha) hii  imefikia hata wachezaji kurogana wenyewe kwa wenyewe ili kujitafutia umaarufu!

Niwazindue viongozi na wachezaji wa timu zetu za kandanda: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili yako yote.”

“Mimi ni BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. Usivisujudie wala kuvitumikia. Imeandikwa: “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu Yeye peke yake. Mche Bwana Mungu Wako: Ndiye Peke Yake Utakayemtumikia.”

Yawezekana kutenda dhambi dhidi ya mapendo ya Mungu kwa namna mbalimbali:*Upurukushani: huzembea au hukataa kujali upendo wa Mungu; kushindwa kutambua uzuri unaoendana nao na kuikataa nguvu yake.*Utovu wa shukrani: hushindwa na kukataa kukiri mapendo ya Mungu na kumrudishia pendo kwa pendo.*Utepetevu: ni kusita au kuzembea kujibu mapendo ya Mungu. Unaweza kuwa ni pamoja na kukataa kujitoa kwa msukumo wa upendo.*Uzembe au uvivu wa kiroho hususia wema wa Mungu.

*Chuki ya Mungu hutokana na kiburi. Ni kinyume cha mapendo ya Mungu ambaye wema wake inaukataa, na ambaye inamdhania kuwa huapiza kama mmoja anayekataza dhambi tu na kutoa adhabu. (Rejea Katekisimu ya Kanisa Katoliki Uk. 470:2093-94).

Wewe mcheza kandanda unayekwenda kwa mchawi ili ‘aisafishe nyota yako’ kwa kumroga mchezaji mwenzako ili aporomoke nawe utwae nafasi yake, uliumbwa na mchawi au Mungu? 

Huyo mchawi alijiumba mwenyewe au Mungu yule yule aliyekuumba wewe? Unapomkana Mungu hapa duniani, kiyama (siku ambayo ulimwengu na kila vilivyomo vitafikia mwisho na wafu watafufuliwa, watasimamishwa mbele ya Mola wao kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa kwa matendo yao duniani) utakuwa mgeni wa nani?

 Ni wajibu wa viongozi wa klabu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukaa pamoja na kutafuta mbinu zitakazozipa mafanikio klabu hizo na Timu za  Taifa katika mechi zake za ndani za za kimataifa badala ya kutegemea uchawi. Vinginevyo tutaendelea kuwa ‘vichwa vya wendawazimu’ na ‘majamvi ya wageni!’ 

Habari Kubwa