Stars imulikwe safu ya ushambuliaji si Manula

07Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Stars imulikwe safu ya ushambuliaji si Manula

TAYARI Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mrundi Etienne Ndayiragige, ameita kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Rwanda kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, CHAN. 

Stars itarudiana na Sudan nchini humo Oktoba 18, mwaka huu ikihitaji ushindi zaidi ya bao 1-0 ili kuweza kufuzu fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon. 

Hiyo ni kutokana na mechi ya awali Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kukubali kipigo cha bao 1-0 jambo ambalo linaifanya Stars kulazimika kupata matokeo zaidi ya hayo ili kuweza kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu 2009.

Hata hivyo, baada ya Ndayiragije kutangaza kikosi chake kitakachoingia kambini kujiwinda na mechi hiyo, kumezuka mjadala mkubwa kutoka kwa wachambuzi na wadau wa soka wakihoji sababu ya kutoitwa kwa kipa wa Simba, Aishi Manula na badala yake kuendelea kumwamini mlinda mlango mkongwe, Juma Kaseja wa KMC FC sambamba na Metacha Mnata wa Yanga. 

Hakuna asiyeukubali uwezo wa Kaseja na zaidi kazi kubwa aliyoifanya hadi kuifikisha Stars katika hatua hiyo kufuatia kuiongoza kuitoa timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars. Katika mchezo huo timu hizo zilitoka sare tasa nyumbani na ugenini kabla Taifa Stars kuvuka kwa mikwaju ya penalti 4-1, huku Kaseja akiibuka shujaa kwa kudaka penalti mbili. 

Lakini pia akafanya kazi kubwa tena dhidi ya Burundi kwenye mechi ya kuwania kufuzu kushiriki hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Katika mechi hiyo ambayo ugenini ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na mchezo wa marudiano Uwanja wa Taifa matokeo yakawa kama hayo, Kaseja aliibuka tena shujaa kwa kucheza penalti hatua ya matuta wakati wakivuka kwa penalti 3-0.

Lakini pia wote tumekuwa mashuhuda kwa uwezo unaoonyeshwa na Mnata katika kikosi cha Yanga hususan kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ambayo kwa sasa wametolewa na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika. 

Kwa mantiki hiyo, Nipashe hatuoni pengo lolote katika nafasi ya kipa kwenye kikosi hicho cha Ndayiragije na badala yake idara ambayo tunaona inahitaji kumulikwa zaidi ni ile ya ushambuliaji. 

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba katika mechi zote tano ambazo Ndayiragije ameiongoza Stars, mbili dhidi ya Harambee Stars na idadi kama hiyo dhidi ya Burundi pamoja na dhidi ya Sudan, tatizo kubwa limekuwa kwenye safu ya ushambuliaji kushindwa kucheka na nyavu. Takwimu haziongopi, dhidi ya Harambee Stars sare tasa nyumbani na ugenini, dhidi ya Burundi bao 1-1 ugenini na nyumbani kabla ya kulala bao 1-0 dhidi ya Sudan Uwanja wa Taifa. 

Kulingana na takwimu hapo, ni wazi safu ya ulinzi ukianzia langoni kwa Kaseja, imekuwa imara zaidi na udhaifu mkubwa umekuwa kwenye ushambuliaji, idara ambayo kama si kumulikwa basi inahitaji mjadala wa kitaifa.

Katika mechi zote tano, washambuliaji wamekuwa wakishindwa kuzitumia nafasi wanazotengenezewa kutoka kwa viungo, jambo ambalo kwa sasa kwetu sisi kusikia wadau wa soka wakianza kuhoji nafasi ya Malula Stars tunaona halina mashiko kabisa.

Hatusemi Manula hana uwezo, bali makipa waliopo wana ubora wa kutosha, hivyo kwa sasa tusimvuruge Ndayiragije tumuache apambane kukisuka kikosi chake na kama ni maoni ya kukiboresha basi kwa mchezaji atakayeweza kuisaidia Stars katika safu ya ushambuliaji.

Habari Kubwa