Umoja Yanga unahitajika sasa, si chokochoko za migogoro

07Oct 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Umoja Yanga unahitajika sasa, si chokochoko za migogoro

TIMU inapotetereka kidogo, kuna baadhi ya wanachama ambao wanakuwa kwenye klabu kimaslahi na kuanzisha chokochoko zao.

Na tayari kuna baadhi ya wanachama wa klabu ya Yanga wamesikika wakianza chokochoko na kumtuhumu Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla kuwa anaipeleka klabu pabaya.

Hii ni baada ya timu hiyo kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pamoja na kutopata ushindi kwenye mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu, ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, na kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania.

Kikubwa zaidi wanadai kuwa hivi sasa haelewani na Makamu wake, Fredrick Mwakalebela.

Wanachama hawa wamekuwa wakisambaza taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii, kiasi cha kuwachanganya na kuwavuruga baadhi ya wanachama wengine wa klabu hiyo.Kwa bahati nzuri, Dk. Msolla mwenyewe amejibu kuwa wanaoeneza habari hizo ni baadhi ya wanachama wakaa milangoni ambao hawajalipwa pesa zao.

Akasema kuwa ni kweli baadhi ya wanachama hawajalipwa, lakini ni suala la muda kwani klabu ina mpangilio wake wa kufanya kazi na kulipa madeni.

"Haiwezekani uache kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi ukawalipe wakaa milangoni. Siyo kama hatutowalipa, lakini kwanza inabidi wasubiri walipwe kwanza wachezaji halafu wengine watafuata," alisema mwenyekiti huyo.

Hapa inaonyesha kuwa ni suala la maslahi tu. Kuna baadhi ya wanachama hawajalipwa, sasa hasira zao wanapeleka kwa mwenyekiti.

Hili ni tatizo ambalo lipo muda mrefu kwenye klabu hizi kubwa za Simba na Yanga. Kuna wanachama ambao kazi yao ni kutengeneza migogoro tu pale wanapoona maslahi yao yameguswa, yapo hatarini au yanacheleweshwa.

Kwa bahati njema tu ni kwamba kwa upande wa Simba suala hili linaweza kuwa ni historia kwa sasa kwani ilipobadilishwa katiba na kwenda kwenye mfumo wa uwekezaji, wanachama wa Simba wamekuwa hawana nguvu ya kikatiba kama ile ya zamani na sasa Yanga imebaki na katiba ile ile ya zamani ambayo mwanachama mmoja tu anaweza kulianzisha ikawa balaa.

Kwa siku za karibuni Yanga imepitia kwenye kipindi kigumu, lakini inaonekana kuna baadhi ya wanachama wanatumia kipindi hiki kutaka kutengeneza mgogoro, badala ya kuwa wamoja na kuangalia wapi walipokosea.

Hii inaonyesha kuwa wapo baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wanapenda timu ifanye vibaya ili wapate fursa ya kuwasema na kuwachafua viongozi wao kwa sababu zao binafsi.

Simba ilitolewa mapema tu kwenye Ligi ya Mabingwa, pamoja na kwamba wanachama na mashabiki waliumia sana, lakini wameendelea kuwa wamoja kiasi kwamba wameanza vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kama kuna tatizo, kuna vikao ambavyo wanachama hukutana na viongozi wao na si kulumbana kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Habari Kubwa