Watumishi 48 kuchunguzwa ubadhirifu

07Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Watumishi 48 kuchunguzwa ubadhirifu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, achunguze watumishi 48 waliojihusisha na upotevu wa fedha kwa njia za udanganyifu.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alitaja maeneo saba ambayo ametaka yafanyiwe uchunguzi wa kina ili kubaini upotevu huo. Eneo la kwanza ni upotevu wa makusanyo ya ndani kupitia mawakala wa ukusanyaji mapato (POS) ambapo mawakala wanaokusanya fedha wanashirikiana na watumishi wa halmashauri na kuzitumia bila kuziingiza benki.

“Kuna kundi la watumishi 10 wakiongozwa na mtu wa Tehama, wameshirikiana kupata ‘password’ na fedha zikishakusanywa wanazitoa na kuzitumia bila kuzipelekea benki. Wamesahau kwamba malipo yalipoingizwa mara ya kwanza, data ilirekodiwa kwenye mfumo wa malipo na sisi tunaona ni kiasi gani kimekusanywa.”

Watumishi hao ni Salum Omari (Mtaalamu wa Tehama); Adam Mzengi (Mhasibu kahamishiwa Gairo); Rafaeli Nasari; Caroline Makundi (kahamishiwa Singida Manispaa), Edson S. Ally (Ofisa Biashara); Martin Kimisho (Mhasibu Msaidizi); Prosper Banzi (Ofisa Biashara); Hassan Ponda (Mhasibu kituo cha afya Ndago); Hafidh Ngayunda (Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya) na Muhidin Mohammed (Mweka Hazina wa Wilaya) ambaye tayari amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma hizo.

Kutokana na upotevu huo, Waziri Mkuu ameagiza Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya akae pembeni hadi uchunguzi wa Takukuru utakapokamilika.

Akibainisha mchezo mwingine uliochezwa na watumishi wa Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu amesema kuna watumishi 38 ambao walilipwa kiasi cha Sh. milioni 46 ambazo zilikuwa sehemu ya Sh. milioni 400 za kujenga vituo vya afya vya Ndago na Kinampanda wilayani humo.

“Hapa nina vocha zote za malipo walipeana fedha watu hawa akiwamo mkurugenzi wao. Lakini ni kazi gani ambayo kundi lote hili lilikuwa likiisimamia na kustahili kupata malipo hayo? Kutoka makao makuu ya wilaya hadi Ndago au Kinampanda kuna umbali gani?” Alihoji Waziri Mkuu.

“Kamanda wa Takukuru fanya uchunguzi, fuatilia wote waliohusika sababu majina tunayo, kama hawastahili kulipwa ni lazima warudishe fedha yetu. Hii ni sehemu ya Sh. milioni 90 ambazo hazijulikani ziliko na zilikuja kujenga kituo cha afya. Fedha hizi zimekuja na maelekezo rasmi, ni kwa nini zilibadilishwa matumizi?” Alihoji.

Habari Kubwa