Wanafunzi wanane mbaroni tuhuma mauaji  mwenzao

07Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
KAHAMA
Nipashe
Wanafunzi wanane mbaroni tuhuma mauaji  mwenzao

WANAFUNZI wanane wa Sekondari ya Seeke mkoani Shinyanga, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia na kusababisha kifo cha mwenzao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao

Mwanafunzi aliyeshambuliwa na baadaye kupoteza maisha ni Constantine Makoye (18), aliyepata majeraha makubwa yaliyosababisha kupoteza maisha wakati wa matibabu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Richard Abwao, alisema shambulio hilo lilitokea Oktoba  29,  saa 12 jioni, katika Kanisa la Wasabato ambako kulikuwa na sherehe ya kuwaaga wanafunzi washirika wa kanisa hilo wanaotarajia kuhitimu kidato cha nne mwezi ujao.

Alisema ugomvi ulitokea siku hiyo, uliibuka baada ya kundi la wanafunzi wakiongozwa na Isaya Athuman (18) wa kidato cha nne na wenzake 10 ambao hawakualikwa kwenye sherehe hiyo, walimvamia Makoye na kuanza kumpiga.

Abwao aliwataja vijana hao kuwa ni Isaya Athuman (18), Godfrey Simon (18), Enock Boniface (18) pamoja na Emmanule  Sekela (18) na wengine wanne majina tunayo kwa vile hawajafikia miaka 18, wote wa Sekondari ya Seeke.

Aidha, alisema baada ya kumvamia walimshambulia huku wakimnyang’anya viatu na maji ya kunywa.

Alisema wanafunzi hao walipiga kelele na mayowe kuomba msaada kuwa wamevamiwa na  kuanza kuwarushia mawe waliovamia hao.

“Baada ya kurushiwa mawe wavamizi hao walikimbia na kutawanyika, lakini Constantine Makoye alizidiwa akiwa amelala chini na wenzake walimtelekeza hadi alipopata nguvu na kwenda nyumbani kumjulisha babu yake ambaye alimpeleka kutibiwa katika hospitali bila kutoa taarifa polisi,” alisema Abwao.

Alisema ilipofika Jumanne wiki iliyopita Makoye alikuwa  hawezi kuongea, ndugu zake walitoa taarifa kituoni poleni na kufungua jalada la kulalamikia  kujeruhiwa kabla ya mwanafunzi kufariki Oktoba 2, katika Hospitali ya Mji wa Kahama.

Kamanda alisema chanzo cha kifo chake ni majeraha makubwa kichwani na kwamba mwili wake umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa taratibu za mazishi.

Habari Kubwa