Mbunge ajitokeza kumrithi Mbowe uenyekiti Chadema

07Oct 2019
Enock Charles
Nipashe
Mbunge ajitokeza kumrithi Mbowe uenyekiti Chadema

VUGUVUGU la uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeanza baada ya Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe, kutangaza nia ya kutaka kuwa mrithi wa Freeman Mbowe.

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe

Kwa sasa chama hicho Mwenyekiti wake ni Mbowe, na kwa mujibu wa Katiba yao wanatakiwa kufanya uchaguzi wa ndani ya chama.

Hivi karibuni, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilikitaka Chadema kuwasilisha maelezo katika ofisi yake kwa kile alichoeleza ni kukiukwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kusogeza mbele uchaguzi wa viongozi wake.

Katika barua hiyo Msajili iliagiza maelezo hayo kuhusu sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huo kuwasilishwa katika ofisi hiyo kufikia Oktoba 7, mwaka huu (leo) saa tisa na nusu mchana.

Akizungumza na gazeti hili kuhusiana na nia yake ya kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini, Mbunge huyo, alisema umefika wakati kwa chama hicho kupata mwenyekiti mpya, kwamba ameamua kugombea nafasi hiyo kwa kile alichodai kuwa na sifa za kuongoza.

“Tunamshukuru Mwenyekiti wetu kwa mambo mengi mazuri aliyokifanyia chama chetu na imefika wakati sasa kuwaachia wengine,” alisema Mwambe.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho Kanda ya Kusini na mjumbe wa Kamati Kuu, alidai kuwa na uwezo wa kuongoza chama hicho baada ya kupata uzoefu wa kuongoza ukanda huo, hivyo sasa anaona anatosha kwa nafasi ya taifa ndani ya chama hicho.

Hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, alisema uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kwa ngazi ya kitaifa unatarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, wiki iliyopita, alinukuliwa akisema kulikuwapo na sababu kadhaa zilizosababisha uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kuchelewa na kufafanua kuwa utafanyika kabla ya kumalizika mwaka huu.

Dk. Mashinji alikuwa anatoa ufafanuzi kuhusiana na barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Habari Kubwa