Rushwa ya ngono bado tishio, tupambane nayo

08Oct 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Rushwa ya ngono bado tishio, tupambane nayo

RUSHWA ya ngono hufanyika kwa siri na baina ya watu wawili kwa anayelazimishwa kutenda hivyo na anayetaka kutenda kwa manufaa yake mwenyewe ili atoe huduma fulani.

Rushwa hiyo iko hata kwenye sehemu za kazi kwamba mtu anatakiwa kutoa rushwa ndiyo apate nafasi ya kazi si kwa uwezo wake, bali kwa rushwa aliyotoa kwa muhusika.

Hilo linakwenda pia hadi kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini kwamba wapo wanafunzi wanaomaliza vyuo na kupewa alama zilizosukumwa na  mahusiano yao na wakufunzi wao kuliko kuwa na uwezo wa masomo hayo.

Hali hiyo imesababisha wanaobebwa kwa kutumia miili yao iwe wanaume au wanawake, kushindwa kufanya kazi inavyopaswa wanapofika katika maeneo yao ya ajira kutokana na ukweli kwamba hawakuwa na sifa ya kupata ajira husika isipokuwa njia ya rushwa waliyoipitia.

Athari kubwa ni kuwa na watu wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa sababu pamoja na mengine mhusika  alitoa rushwa ya ngono ili afaulu kwa kiwango cha juu.

Yaani apate ufaulu (GPA) ya daraja la kwanza, na hivyo hivyo alipofika kazini akatoa rushwa nyingine ili apate nafasi na hata alivyopata nafasi hiyo akaendelea kutoa rushwa ili ajihakikishie nafasi yake.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imethibitisha kuwa rushwa ya ngono ni ngumu kukabiliana nayo, kutokana na mazingira ya utendekaji wake na wahusika.

Aidha, wakati mwingine wahusika hawatoi taarifa kwa mamlaka zinazohusika kutokana na sababu mbaalimbali.

Baadhi ya sababu hizo ni kwa mhusika kuchukulia kwamba ikitoa taarifa atadhalilika au kushusha heshima yake iwapo jambo hilo litajulikana.

Wengine ni kutokana na utamaduni wa usiri na mfumo dume na hivyo wamejikuta wakishindwa kupaza sauti.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli, alisema rushwa ya ngono kwa wanaume ipo pia kwani wapo wanaohongwa na wanawake, jambo ambalo limeleta changamoto katika utekelezaji wa majukumu.

Rushwa ya ngono ni kati ya makosa 24 yanayoshughulikiwa na sheria ya rushwa ya Takukuru, na wapo ambao wamechukuliwa hatua baada ya kukamatwa.

Rushwa hii ina athari nyingi ikiwa ni pamoja na kudidimiza taifa kwa kuzalisha watu wasielimika, wasio na uwezo wa kutenda kazi na ofisi kukosa ufanisi kwa sababu mapenzi yanakuwa ndiyo kipaumbele.

Lakini changamoto nyingine ni kuongeza maambukizi ya maradhi mbalimbali, kwa sababu baadhi ya wanaojenga mazingira ya rushwa hiyo kutendeka wanajua uhalisia wa afya zao kwamba zina walakini, hivyo kuendeleza maambukizi kwa wengine.

Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kinafanya kampeni ya kuelimisha jamii kutambua madhara ya rushwa ya ngono na athari zake, pia kuibua habari mbalimbali ambazo zitasaidia kuwabaini wanaohusika na matukio hayo.

Kwa ujumla janga hili linadidimiza taifa na kusababisha watu wasipate huduma stahiki. Aidha, linaongeza wasio na sifa na kuwanyong’onyesha wenye sifa za nafasi husika.

Wakati tukielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ni muhimu kuitazama kwa jicho la pekee rushwa hii, kwani inafifisha azma ya kupata viongozi sahihi ambao watawatumikia wananchi.

Yeyote anayekutwa na rushwa ya ngono atambue kuwa ni kosa kisheria na inaweza kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Ni faraja kutokana na taarifa njema kwamba Takukuru ina namna ya kuwahudumia wanaokumbwa na adha hiyo na kwamba taarifa zao zitabaki kuwa za siri.

Muungwana anaona kwamba kama mamlaka zimejitokeza kukabiliana na rushwa hiyo sehemu mbalimbali nchini, basi ni wajibu kwa wanaonyanyasika kwa namna yoyote vya rushwa hii wakatoa taarifa na hatua zikachukuliwa.

Jamii ikishiriki kutokomeza rushwa hii maana yake nafasi za ajira zitapata watu sahihi, wasomi sahihi na wananchi sahihi ambao hawategemei kutoa kitu au kujidhalilisha ili kupata nafasi fulani.

Habari Kubwa