Tuamue sasa kuhusu kutumia simu shuleni

08Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tuamue sasa kuhusu kutumia simu shuleni

WIKI iliyopita shule ya Sekondari ya Kiwanja, iliyoko mkoani Mbeya ilichomwa moto na wanafunzi zaidi ya 13 wanaodaiwa kuwa walighadhabika kutokana na simu zao kuchukuliwa na uongozi wa shule hiyo

Suala la simu shuleni, si kitu cha kukipuuza kwa sababu tupende tusipende ni vigumu kuwadhibiti wanafunzi wasiingie na simu mabwenini au shuleni kwani wanafahamu wenyewe cha kufanya kumiliki simu hizo. 

Vuguvugu la wanafunzi kuruhusiwa kutumia simu shuleni au kuzipiga marufuku kuingiza  eneo hilo  ni jambo ambalo linahitaji wadau kulizungumza ili kuepusha yale yaliyotokea Sekondari ya Kiwanja.

Vita vya simu shuleni havina mshindi hata kama zitakatazwa wanafunzi wanajua namna ya kuziingiza na kuzitumia bila kugundulika na walimu na watakapobainika na kuzuiliwa si kwamba tatizo hilo litamalizika.

Kwa vile ni vigumu kukataza simu shuleni zama hizi, wakati huu kwani ni nyenzo muhimu ya mawasiliano miongoni mwa watoto wawe sekondari au shule za msingi kwa hiyo zinahitajika sheria na miongozo ya namna ya kumiliki na kutumia simu shuleni.

Tunaona kuwa wanafunzi wanahitaji simu kwa sababu ya kusoma na pia kuwasiliana na familia zao na walimu pia.

Pia simu hiyo ni nyenzo ya kusomea na kujifunzia , kwa hiyo inahitajika miongozo na taratibu za kutumia simu shuleni.

Pengine ni wakati wa kufikiria, hasa wadau na  Wizara ya Elimu kuona namna ya kuandaa miongozo na sharia hizo na shule zikaanza kuruhusu wanafunzi kutumia simu.

Lakini ni vigumu kusema kuwa kama taifa tupige marufuku matumizi ya simu shuleni.

Tunaona kuwa zama hizo simu ni nyenzo ya kusomea na kujifunzia. Simu zinaweza kutumiwa kupakua vitini kwenye mtandao ni jambo ambalo halikwepeki. Shule nyingi hazina kompyuta lakini zinaweza kuruhusu wanafunzi kutumia simujanja kupakua vitini na elimu kutoka kwenye mitandao mbalimbali.

Wanafunzi watumie intanet kusoma na kwa wale ambao hawana simujanja na fedha za kuchukua vitini , shule italazimika kuwa na kompyuta ndogo (mpakato) kwa ajili ya kupakua vitini mtandaoni.

Lakini si hivyo tu kuna mkongo wa taifa ambao unategemewa kusambaza mtandao wa intanet nchi nzima, ndiyo wakati wa shule nazo kutoa ‘vifurushi vya wifi’ bure kwa wanafunzi ili wanapopakua vitini viwafikie wanafunzi wote kwa kuwa shule inagharamia kwenye simu na kwenye kompyuta ya simu.

Wanaweza kupakua kutoka kwenye google na Wikipedia. Hizi ni zama za sayansi na teknolojia huwezi kukwepa teknolojia ya simu ni vyema kulitafakari hili na kulifanyia maamuzi.

Tunaona kuwa simu zina umuhimu wa kipekee shuleni. Kwa mfano ni nyenzo ya mawasiliano baina ya wazazi na watoto.

Simu zinaweza  kutumia kuwahakikishia ulinzi wa watoto na utaratibu huu unawezekana kwenye simujanja (smartphones) na hivyo itasaidia kunasa na kufahamu kuhusu watoto watukutu kama wapo shule au wameingia mitaani.

Simu hizo pamoja na mambo mengine zinaweza kutumika kuwasiliana wakati wa dharura. Mathalani kuna uvamizi, ubakaji watoto, yapo mashambulizi  na hata utoroshaji wa albino.

Simu kama nishati ya umeme zinahitajika shuleni. Kwa hiyo ni vyema kuandaa utaratibu na muda wa kuzitumia badala ya kufikiria kuzipiga marufuku.

Ndiyo maana tunasema ni vyema shule zikaandaa namna bora ya kutumia simu badala ya kuzipiga marufuku.

Suala la usalama wakati wa kuchaji simu nalo ni la muhimu hivyo, ili kuepusha hatari ya kuleta shoti na umeme au kutokea milipuko kutokana na kutumia chaja mbovu shule ziweke mazingira bora ya kuchajia.

Habari Kubwa