Utata bao la Yanga SC vs Coastal ulipo

08Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Utata bao la Yanga SC vs Coastal ulipo
  • ***Mshika kibendera namba mbili atajwa, kwa nini linapigwa? VAR yamulikwa huku...  

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Yanga, kwa mara ya kwanza msimu huu juzi waliandika ushindi wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union kwa bao pekee lililozua utata kwa wachezaji wa timu-

-pinzani, mashabiki, wadau wa soka na wachambuzi wa mchezo huo nchini.

Katika mechi hiyo ya tatu kwa Yanga msimu huu, iliyopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, vijana hao wa Kocha Mwinyi Zahera, walipata bao lao dakika ya 51 kupitia kwa Abdulaziz Makame ambalo lilidumu kwa dakika zote 90 na kuifanya timu hiyo kushinda kwa bao 1-0.

Hata hivyo, bao hilo lilizua utata mkubwa huku wengi wakidai mwamuzi wa kati na yule wa akiba hawakuwa makini na walilikubali kimakosa kwa sababu mpira ulikuwa  haujavuka mstari wa golini.

Bao lilivyofungwaUlikuwa mpira wa kona uliopigwa na winga Mrisho Ngassa dakika ya 51 na kumkuta beki wa Yanga Ali Ali aliyeachia krosi iliyotua kichwani kwa Makame ambaye aliiunganisha langoni mwa Coastal Union, lakini ikamkuta mmoja wa mabeki wa timu hiyo na kuucheza kwa kichwa.Hata hivyo, mwamuzi wa mchezo huo, Abubabar Mturo kutoka Mtwara aliamuru mpira kutengwa katikati ya dimba la Uhuru kwa kuwa lilikuwa ni bao halali kutokana na beki aliyeokoa kuucheza mpira huo ukiwa umezama kimyani.

Wachezaji wa Coastal Union walimlalamikia refa Mturo wakidai mpira uliokolewa kabla ya kuvuka mstari wa goli, jambo ambalo pia mashabiki wengi na wachambuzi wa soka waliamini hivyo na umeendelea kuwa mjadala mkubwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii.

Utata ulipoKwanza kabisa wachezaji wa Coastal, walisita kumbughudhi ipasavyo Makame kufuati mshika kibendera namba mbili, Credo Mbuya kunyosha kibendera juu kabla ya Makame kuunganisha golini kwa kichwa akiashiria mchezaji huyo alikuwa ameotea.

Hata hivyo, kabla ya Makame kuucheza kwa kichwa Mbuya alishusha kibendera chini baada ya kubaini kuwa langoni mwa Coastal Union kulikuwa na beki aliyerudi nyuma wakati kipa wao, Soud Abdallah alipokuwa mbele kuwania kudaka mpira, hivyo moja kwa moja hapakuwa na kuotea.

Pili kuhusu beki wa Coastal Union, kabla ya kuucheza mpira huo alikuwa kwenye mstari wa golini na kisha mpira ulipopigwa alirudi ndani ya goli na kuu kuucheza, utata hapo unakuja kwamba akiucheza mpira  mwili ulikuwa ndani ya goli lakini mpira ulikuwa haujavuka mstari.

Kutokana na ukweli kwamba kitendo kile kilikuwa cha haraka sana, kwa mujibu wa mchambuzi wa Azam TV, Ally Mayay, anasema: "Ni kweli wakati anaucheza mpira huo alikuwa katika mstari, lakini ili kuucheza mpira alirudisha kichwa ndani ili kuvuta kasi na wakati huo mpira ulishavuka mstari."

Ni refa au mshika kibendera?Kutokana na eneo alilokuwa refa, Mturo ni wazi mshika kibendera namba mbili, Mbuya jicho lake ndilo lilikuwa sahihi kabisa kukubali ni bao ama si bao kwa kuwa alikuwa usawa wa mstari wa mwisho unaotoka moja kwa moja golini, hivyo kulikubali ama kulikataa yeye ni muhusika sahihi.

VAR ni muhimu?Utata kama huu ndio uliochangia kuwapo kwa Teknolojia ya Msaada wa Video kwa Refa (VAR) kwa baadhi ya Ligi Kuu Ulaya na michuano ya kimataifa, hivyo kama ingekuwa inatumika Ligi Kuu Bara pasingekuwapo na sintofahamu hiyo.

Nafasi ya Yanga, CoastalKwa matokeo hayo Yanga iliyoshuka dimbani mara tatu inakwea hadi nafasi ya 12 kutoka mkiani kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 20 ikiongozwa na Simba iliyoko kileleni kutokana na kushinda mechi zake zote nne wakati Coastal Union yenyewe ipo nafasi ya 15.

Ligi hiyo kwa sasa imesimama kupisha Kalenda ya Fifa na itaendelea tena Oktoba 23, mwaka huu kwa michezo mbalimbali kupigwa.

Habari Kubwa