Stars yachelewesha rungu Mkude Simba

08Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Stars yachelewesha rungu Mkude Simba

UONGOZI wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, umesitisha kutoa uamuzi juu ya hatima ya kiungo wake, Jonas Mkude, imefahamika.

Jonas Mkude

Mkude anakabiliwa na makosa ya utoro, ambayo yalisababisha akakosekana katika msafara wa timu hiyo uliokwenda mikoa wa Kanda ya Ziwa (Kagera na Mara), kwa ajili ya kucheza dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United.

Taarifa zilizopatikana kutoka uongozi wa Simba zinaeleza kuwa, tayari Mkude alishafika kwa uongozi na kujitetea, pamoja na viongozi wa benchi la ufundi nao walitoa taarifa zao kuhusu kiungo huyo.Chanzo chetu kimesema kuwa, uongozi ulitarajia kutoa uamuzi jana, lakini wakasimamisha mchakato huo kutokana  na nyota huyo kuwa katika kambi ya timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo inajiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Rwanda.

"Suala la Mkude limesimama kwa muda kwa sababu ya kuitwa katika kikosi cha Stars, hukumu yake ilikuwa itolewe leo (jana) Jumatatu, lakini ameshajieleza na sisi viongozi wa timu, pia tulitoa taarifa kwa upande wetu, " kilisema chanzo chetu.

Wakati huo huo, kikosi cha mabingwa hao watetezi kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC utakaochezwa Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Taarifa zaidi kutoka katika klabu hiyo zimeeleza kuwa uwezekano wa kwenda Kigoma kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Aingles kutoka Burundi uko katika hatihati kutokana na maandalizi ya mchezo huo kutokamilika.

"Leo (jana) tumefanya mazoezi, na kesho (leo), ratiba yetu inaendelea kama kawaida, kama ni kusafiri ilipaswa tusafiri kesho (leo), na mpaka muda huu hakuna taarifa rasmi, nadhani huo mchezo hautafanyika," chanzo chetu kilisema.

Chanzo hicho kilisema kuwa ni kweli Kocha Mkuu Mbelgiji Patrick Aussems alihitaji mechi mbili za kirafiki kabla ya kuivaa Azam FC, lakini bado mazungumzo hayajafikia mwisho na timu za kucheza nazo.

Habari Kubwa