Maxime alia gundu kuwagubika Kaitaba

09Oct 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Maxime alia gundu kuwagubika Kaitaba

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amesema kwa sasa timu yake imekuwa na bahati mbaya kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kaitaba, hivyo anajipanga upya kusaka dawa ya ushindi.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime

Akizungumza na gazeti hili jana, Maxime, alisema tangu ameifunga Simba mechi ya msimu uliopita, Kagera Sugar haijapata ushindi ikiwa nyumbani.

Maxime alisema wachezaji wake wanapambana na kucheza kwa bidii, lakini wanashindwa kufunga na hivyo kujikuta wanapoteza ushindi na kuacha wapinzani wao wakiondoka na pointi tatu.

"Yaani kwa sasa mambo ni magumu tukiwa nyumbani, tumefungwa mechi saba mfululizo, tangu tulipoifunga Simba mchezo wa msimu uliopita, hatujashinda, wakatufunga wengine na baada ya kutufunga hapa majuzi, tukafungwa tena na JKT Tanzania," alisema Maxime.

Aliongeza kuwa msimu huu ligi ni ngumu zaidi, hivyo wataendelea kurekebisha makosa na hatimaye kuvuna pointi na kujiweka mahali pazuri katika msimamo wa ligi.

"Siku hizi hakuna faida ya uwanja wa nyumbani, kuna matokeo mengi ya kushangaza, halafu mara nyingi timu inayocheza mpira mkubwa, huwa haipati matokeo, kikubwa makocha tunatakiwa kuendelea kuwaweka vizuri wachezaji ili wasitoke mchezoni, " alisema kocha huyo.

Kagera Sugar imecheza mechi nne na ina pointi tisa katika msimamo wa ligi hiyo unaoongozwa na mabingwa watetezi Simba wenye pointi 12.

Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa imesimama kupisha kalenda ya kimataifa ya Fifa ambapo Timu ya Taifa (Taifa Stars) yenyewe imeingia kambini kujiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda itakayochezwa Oktoba 14, mwaka huu jijini Kigali.

Habari Kubwa