Azam hakuna kulala hadi kieleweke Simba

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Azam hakuna kulala hadi kieleweke Simba

KIKOSI cha Azam FC kitaendelea na mazoezi yake bila kupumzika kwa ajili ya kujiweka imara kuwakabili Simba, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffer Idd

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffer Idd, alisema jana lengo la kutovunja kambi ni kutaka kuwaimarisha wachezaji wao kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Iddi alisema wanataka kuingia katika mchezo huo kwa lengo moja la kupata ushindi na kujifuta machozi ya kupoteza pointi nne katika msimu uliopita dhidi ya mabingwa hao watetezi.

"Timu ilipewa mapumziko ya siku moja baada ya kumaliza mchezo dhidi ya Namungo, kwa sasa itaendelea na kambi mpaka tutakapocheza na Simba, tunasisitiza kila mechi kwetu ni muhimu na tunahitaji kuonyesha kwamba msimu huu tumeingia kivingine," aliongeza Idd.

Alisema wanahitaji kuvuna pointi nyingi msimu huu ili wakate tiketi  ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani wenyewe na si kwa kusubiri "mbeleko".

"Tunaijua Simba na wao pia wanatujua, tunaamini tutapata matokeo mazuri tutakapokutana, matokeo ya msimu uliopita yameshakuwa historia, sasa tunaangalia mchezo uliopo mbele yetu," alisema kiongozi huyo.

Simba na Azam FC zote zimeshatolewa katika mashindano ya kimataifa na nguvu na akili zao zimeelekezwa kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania itakayoanza baadaye mwaka huu.

Habari Kubwa