Simba yafuata dawa Azam kwa Warundi

09Oct 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Simba yafuata dawa Azam kwa Warundi
  • ***Yatangaza mechi tatu kali za kirafiki ikianza na Wakenya Taifa Jumamosi, huku Aussems akisema...

KOCHA Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amesema lengo la kuomba timu yake icheze mechi za kirafiki ni kutaka kuwaongezea "kasi" na kuwaimarisha wachezaji ili wafanye vema katika mbio za kutetea taji-

-hilo wanalolishikilia hususan mechi iliyopo mbele yao dhidi ya Azam FC.

Simba inatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Bandari kutoka Kenya itakayochezwa keshokutwa, Jumamosi halafu Oktoba 14, mwaka huu itawafuata Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma na baada ya siku mbili itakutana na Aigle Noir ya Burundi kwenye uwanja huo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aussems, alisema kuwa mechi hizo zitakuwa sehemu ya mazoezi na anatarajia kutumia wachezaji wote waliobakia baada ya wenzao kuitwa kwenye timu zao mbalimbali za taifa.

Aussems alisema anahitaji kuona wachezaji wake wanacheza mechi hizo katika kiwango bora kwa sababu wanajiandaa kukutana na Azam FC ambayo pia ina kikosi imara.

Mbelgiji huyo alisema kuwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ni ngumu na hakuna klabu inayoingia uwanjani ikiwa imejiamini inaondoka na ushindi, mpaka pale dakika 90 zitakapomalizika.

"Ni ligi ngumu, ni ligi yenye ushindani, kila timu inaamini inaweza kupata ushindi na hakuna mchezaji anayekata tamaa, hii inatufanya tujipange na kuendelea kujiimarisha ili tuweze kutimiza malengo, naamini kwamba kila mechi ni sawa na fainali," alisema Aussems.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wamekubali mwaliko wa kwenda Kigoma kwa sababu ya kuendelea kuwajenga wachezaji na vile vile kuwaweka karibu na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo walioko mkoani humo.

"Tunajua Kigoma haina timu ya Ligi Kuu, lakini ina mashabiki wa Simba, hii ni zamu yao, wajiandae kutupokea, watapata nafasi ya kuwaona wachezaji wao kwa karibu," Aussems alisema.

Baada ya mechi hizo za kirafiki, Simba watarejea jijini Dar es Salaam kuwasubiri Azam FC kwa ajili ya kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Oktoba 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba iko kileleni ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi nne, wakati watani zao, Yanga ambao wameshuka dimbani mara tatu wana pointi nne kufuatia kupoteza mchezo mmoja, kushinda mmoja na sare mmoja.

Habari Kubwa