Zahera awatamani Waarabu droo Caf

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Zahera awatamani Waarabu droo Caf

WAKATI leo Yanga ikiwa katika uwezekano wa kuangukia kuvaana na Waarabu wa Misri, Pyramids ama wa Algeria, Paradou AC, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, amesema haihofii timu-

-yoyote kwenye droo hiyo ya mechi za mchujo kuwania kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga imeangukia kucheza mechi ya mchujo baada ya kutolewa na Zesco ya Zambia kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo droo ya mechi hizo za mchujo zitachezeshwa jijini Cairo, Misri leo.

Mbali na timu hizo mbili za Uarabuni, pia Yanga inaweza kupangwa kukutana na ESAE ya Benin, DC Motema Pembe (DRC), FC San Pedro (Ivory Coast), Bandari (Kenya), Bidvest Wits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) ama Triangle United ya Zimbabwe.

Zahera alisema soka la Afrika limebadilika kwa sasa, kwani viwango vya wachezaji vinafanana hali inayompa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi hiyo ya mchujo.

Alisema amejifunza mambo mengi kutokana na kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, na kwamba atarekebisha makosa waliyoyafanya ili yasijitokeze Kombe la Shirikisho.

“Soka la Afrika hivi sasa limebadilika kwa kiwango kikubwa, awali timu nyingi zilikuwa zinazihofia timu za Waarabu, lakini hivi sasa hawaziogopi kutokana na ubora wao kupungua. Hivyo tupo tayari kukutana na timu yoyote kutoka Uarabuni, na nina uhakika wa kupata matokeo mazuri nyumbani na ugenini,” alisema Zahera.

Habari Kubwa