Mchenga mabingwa tena Sprite Bball Kings 2019

10Oct 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mchenga mabingwa tena Sprite Bball Kings 2019

BAADA ya upinzani mkali kutanda katika fainali tatu zilizopigwa jijini Dar es Salaam, hatimaye timu ya mpira wa Kikapu ya Mchenga Bball Stars, imeendeleza ubabe kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Sprite Bball Kings 2019, hii ikiwa ni mara ya tatu mfululizo.

Mabingwa wa mpira wa Kikapu, timu ya Mchenga Bball Stars wakiwa na mfano wa hundi ya Sh. milioni 10 baada ya kutwaa ubingwa wa Sprite BBall Kings 2019 juzi, hii ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kubeba taji hilo. PICHA: SABATO KASIKA.

Mchenga imetwaa ubingwa baada ya kufanikiwa kushinda mechi ya tatu ya fainali dhidi ya Tamaduni, iliyochezwa juzi katika Uwanja wa Don Bosco Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Mchenga Bball Stars ilishinda kwa vikapu 115 dhidi ya 109 vya Tamaduni, na hivyo kufanikiwa kutetea ubingwa huo ambao timu hiyo inaushikilia kuanzia  mwaka 2017.

Kwa kubeba ubingwa huo, Mchenga Bball Stars  imejinyakulia kitita cha Sh. milioni 10 za Kitanzania, huku mshindi wa pili ambaye ni Tamaduni akijinyakulia kitita cha Sh. milioni tatu.

Katika fainali ya mchezo wa kwanza iliochezwa Ijumaa iliyopita, kwenye viwanja vya Don Bosco, Mchenga Bball Stars ilivutwa shati na kupata ushindi mwembamba wa vikapu 122 dhidi ya 121 vya Tamaduni.

Baada ya hapo ikafuata fainali ya mchezo wa pili iliofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, Mchenga Bball Stars ikaongeza kasi zaidi na kuibuka na vikapu 104 dhidi ya 89 vya Tamaduni.

Msemaji wa mchezo huo, Goza Chuma alisema, fainali ya mchezo wa tatu iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Don Bosco, Tamaduni ilijiuliza tena na kujikuta ikipata kichapo cha vikapu 115 kwa 109.

"Mchenga imetwaa ubingwa kwa mara nyingine baada ya kufanikiwa kushinda kwenye fainali zote tatu dhidi ya Tamaduni, kwa hiyo hao ndio mabingwa wa Sprite Bball Kings 2019," alisema Goza.

Goza alisema, michuano hiyo ya Sprite Bball Kings 2019, ambayo ilihitimishwa rasmi juzi, iliandaliwa na East Africa TV na East Africa Radio kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite.

Habari Kubwa