Mkude kuendelea kuula Taifa Stars

10Oct 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Mkude kuendelea kuula Taifa Stars

HUKU kukiwa na taarifa kuwa uongozi wa Simba umemfungia kwa muda kiungo wake, Jonas Mkude, kutokana na kosa la utovu wa nidhamu, Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Juma Mgunda, amesema kwamba adhabu hiyo hawaitambui.

Mkude na kiungo wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Clatous Chama, wanadaiwa kusimamishwa kwa muda usiojulikana baada ya kubainika walichelewa kuamka na hivyo kushindwa kusafiri na kikosi cha timu hiyo kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa (Kagera na Mara).

Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi zilizotolewa na uongozi wa Simba, lakini imefahamika kwamba nyota hao wawili walishapeleka utetezi wao kuhusiana na makosa yanayowakabili.

Mgunda aliliambia gazeti hili kuwa Mkude anaendelea vema na mazoezi ya timu hiyo inayojiandaa kuwafuata Rwanda kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa unayotarajiwa kuchezwa Oktoba 14, mwaka huu jijini Kigali.

Kocha huyo alisema adhabu hiyo ya klabu yao hawaitambui, na wanachoangalia ni mwenendo wake ndani ya kikosi hicho.

"Sisi hatuna taarifa hizo za kufungiwa, kwa upande wetu hakuna kosa ambalo amefanya, yupo hapa kambini kwa wakati, anafanya mazoezi kikamilifu pamoja na wenzake, hatuwezi kuyaingilia yaliyopo kati yake na klabu yake," Mgunda alisema.

Kikosi cha Stars kinatarajia kuondoka nchini Jumamosi na kinatarajia kutumia mchezo huo ili kujiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), dhidi ya Sudan itakayochezwa Oktoba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa El Merreikh Omdurman.

Habari Kubwa